Dar es Salaam
MATUMIZI ya tumbaku katika umri mdogo husababisha athari za mapema za kuzorota kwa afya ya akili, mapafu, ukuaji na mwili mzima kuathirika kwa kiasi kikubwa hivyo kuchangia upotevu wa nguvu kazi katika taifa.
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Mwanaada Kilima akielezea Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku ambayo huadhimishwa Mei 31 kila mwaka ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa watu wote kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku, kuongeza msukumo kwa watunga Sera na mamlaka mbalimbali ili kuendeleza zuio la matumizi ya tumbaku.
Amesema, kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zimebaini kuwa watoto ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya tumbaku na sigara.
“Matumizi ya sigara yapo katika mfumo ambao unawarubuni watoto na vijana ambapo bidhaa hizo zipo katika namna ya ushawishi na mifumo mbalimbali ya kieletroniki kama bomba au saa,” amefafanua Dk. Kilima.
Dk. Kilima ameongeza matumizi ya tumbaku na sigara husababisha vifo na mdhara makubwa ya afya hivyo huchangia magonjwa yasiyoambukizwa ambapo asilimia tisini ya uvutaji wa sigara husababisha saratani mbalimbali ikiwemo saratani ya mapafu, saratani ya shingo na kichwa, saratani ya tumbo, shinikizo la juu la damu, kiharusi, mshtuko wa moyo, maradhi ya akili n.k
Aidha ametoa wito kwa vijana, watoto na watu wote kuacha matumizi ya tumbaku na aina zozote za sigara ikiwemo sigara za kielektroniki na nyinginezo maarufu kama (shisha) kwani matumizi yake kwa saa limoja ni sawa na kuvuta sigara mia moja na kuleta madhara makubwa.
Kauli mbiu ya siku ya kutotumia Tumbaku mwaka huu ni “Tuwalinde watoto dhidi ya urubuni wa makampuni ya tumbaku”.