Home BIASHARA SERIKALI YAPUNGUZA KODI KWENYE VIFAA VYA MAZOEZI TIBA

SERIKALI YAPUNGUZA KODI KWENYE VIFAA VYA MAZOEZI TIBA

Na Saidina Msangi, Dodoma.

SERIKALI imesema kuwa msamaha kwenye vifaa tiba vya mazoezi yaani physiotherapy hutolewa kwa hospitali zilizosajiliwa na kuidhinishwa na Waziri wa Afya, ambapo hupatiwa msamaha wa kodi kwa lengo la kuboresha afya kupitia mazoezi, ambayo ni njia bora ya kuzuia magonjwa na kuboresha ustawi wa jumla wa jamii.

Hayo yameelezwa leo Mei,28 2024 bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Sylvia Fransis Sigula, aliyetaka kujua kuhusu Serikali kupunguza kodi kwenye Vifaa vya Mazoezi kwa kuwa mazoezi ni tiba.

Chande amesema kuwa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, kama ilivyofanyiwa marekebisho mbalimbali, imeainisha msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika kipengele cha 6(1) na Jedwali la misamaha lililopo kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ambapo bidhaa au huduma zilizopewa msamaha wa Kodi ya VAT ni pamoja na vifaa vinavyotumiwa kwa ajili ya tiba.

‘‘Kuhusu kuondoa kodi kwenye vifaa vyote vya mazoezi ushauri umechukuliwa na unaenda kufanyiwa kazi kwani Serikali iko kwenye mchakato wa ukusanyaji wa maoni na hatimaye kutungwa sheria baadaye kupitishwa bungeni, kwa sasa tuangalie zaidi vyanzo vya ukusanyaji mapato kuliko kupunguza vyanzo vya mapato,’’ amefafanua Chande.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here