Home AFYA CHUO CHA UFUNDI FURAHIKA KIMEJIPANGA KUWAKATIA BIMA YA AFYA WANAFUNZI

CHUO CHA UFUNDI FURAHIKA KIMEJIPANGA KUWAKATIA BIMA YA AFYA WANAFUNZI

Na Sophia Kingimali @Lajiji Digital

CHUO cha Ufundi cha Furahika kimejipanga kuwakatia Bima ya Afya wanafunzi wake wanaochukua kozi za mwaka mmoja ili kuwapa utulivu wa kutafuta matibabu wanapopata changamoto ya maradhi pindi wawapo chuoni hata wanapomaliza na kuanza kutafuta kazi au kujiajili.

Akizungumza leo Mei 24, 2024 chuoni hapo, Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa chuo hicho Dk. David Msuya, amesema kuwa kwa awamu ya kwanza ya mradi huo wafadhili wamepanga kuanza na bima kwa wanafunzi 30 na siku zijazo idadi hiyo itaongezeka kulingana na mahitaji.

“Haya kwetu ni mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa chuo hiki mwaka 2021, hivyo tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wetu mpendwa, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango kwa wawekezaji kuja nchini kuunga mkono juhudi za maendeleo hususan katika nyanja ya elimu.

“Hivyo naomba wazazi waendelee kuleta watoto wao hapa ambapo kutokana na mradi wa elimu bure, vijana wao watapata mafunzo bila malipo ingawa wao watakacholipia ni shilingi 50,000 tu kwa ajili ya mtihani wa mwisho unaosimamiwa na mamlaka nyingine za elimu,” amesema.

Pia Dk. Msuya amesema wapo katika mchakato kutoa ufadhili wa masomo ‘Scholarship’ kwa wanafunzi ambao wamepita na walipo katika chuo hicho kwenda kuongeza elimu zaidi nje ya nchi kwa aliyefikisha vigezo ikiwemo kupata alama za masomo zinazohitajika.

Ameongeza kuwa kinachotakiwa ni wanafunzi kuongeza juhudi ya kufanya vizuri katika masomo yao ili Shirika la Furaha lenye makao yake makuu jijini Dodoma,litakapoleta nafasi hizo za masomo nje ya nchi ziwakute vijana wenye vigezo wakiwa tayari wakisubiri muda tu.

Aidha Dk. Msuya amesema kuwa wapo katika mkakato wa kuanza kutoa mafunzo ya uuguzi ya mwaka mmoja lengo likiwa kuisadia serikali katika sekta ya afya kwani wanafunzi watakaohitimu wataenda kufanya kazi ya kujitokea katika Hospitali za Serikali, huku Shirika la Furahika litakuwa likiwahudumia kwa posho, malazi na chakula kwa kipindi chote watakachokuwa wakitoa huduma hiyo.

“Tumeshatuma maomba serikalini ili kuanza kutoa mafunzo hayo ya uuguzi bure na pindi tutakapokubaliwa mchakato huo utaanza haraka kwa kuanza usaili wanafunzi wa kozi hiyo ila kwa sasa tunaendelea na usaili wa wanafunzi wa kozi ya Ushonaji, Hoteli, Compyuta, IT, Udereva, Umeme,Bandari na mwisho wa kupokea maombi ni Julai 3, mwaka huu.

“Tunatoa wito kwa wazazi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwaleta vijana wao kupata elimu bure kwa kozi wanazotaka ili kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika nyanja ya elimu kwa kufanikisha ndoto za watoto ambao wamekosa fursa ya kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali za kimaisha,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here