Na Sophia Kingimali, @Lajiji Digital
MKURUGENZI Kituo cha Kulelea Watoto Mount Zungwa Day care na kada wa chama cha mapinduzi (CCM), Anania Mwigavile ametoa rai kwa wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita ya kuboresha sekta ya afya nchini kwa kujitolea kwa hali na mali katika kuboresha na kulinda miundombinu katika sekta hiyo.
Wito huo ameutoa leo mei 23,2024 jijini Dar es salaam wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo sementi pamoja na vifaa vya usafi na maji ya kunywa katika zahanati ya Kwembe kati iliyopo mtaa wa Njeteni kata ya kwembe wilaya ya ubungo.
Amesema jamii inapaswa kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia umma lakini pia kujiwekea utaratibu wa kujitolea katika kusaidia maendeleo katika mitaa yao.
“Mimi nimejitolea hiki kwa ajili ya kusaidia hospitali yetu ili iweze kukamilisha ujenzi wa eneo hili la huduma ya wamama na watoto ili waweze kupata huduma ya afya nzuri kama hospitali nyingine hiki ni kidogo nihamasishe na wengine kujitolea ili kuhakikisha watoto wetu wanapata hapa huduma katika mazingira mazuri,” amesema.
Mwigavile amesema kuna haja ya wazazi kuwafundisha watoto kwa vitendo katika kusaidia na kujitolea kwa jamii ili waweze kuwa msaada wa baadae kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Tumekuja hapa na watoto wa kituo chetu cha Mount Zungwa ili wajifunze kwa vitendo kutoa na kusaidia ili hata baadae pamoja na serikali kufanya lakini na wao wawe na uthubutu wa kujitolea,”amesema.
Kwa Upande wake mtendaji wa Mtaa wa Njeteni Frank Mkali amemshukuru kada huyo kwa kujitolea kwake kwa maendeleo ya mtaa na hasa hospitali ambayo imekuwa ikihudumia wananchi wengi wa mtaa huo na wengine kutoka pembezoni.
Amesema bado mambo yanayotakiwa kufanyika katika maendeleo ya mtaa ni mengi ikiwemo barabara za ndani hivyo ametoa rai kwa wananchi wa mtaa huo kuendelea kujitolea kwa hali na mali kushirikiana na serikali ili kuhakikisha mtaa unakuwa na maendeleo.
Naye,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mtaa wa Njeteni, Esther Kitundu amesema chama kitaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha maendeleo ya mtaa huo yanakua ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama.
“Maendeleo yanaanzia nyumbani hivyo jamani tunapaswa kujitolea kwa ajili ya mtaa wetu bila kujali maneno watu watasema nini popote kwenye maendeleo maneno hayakosekani sasa hatupaswi kurudi nyuma bali tushirikiane ili kuhakikisha tunaleta maendelo kwenye mtaa wetu,”amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajumbe wa chama hiko katika ngazi ya mtaa wamesema maendeleo ya mtaa yanaanza na wakazi wenyewe hivyo ni vyema wananchi kushiriki katika kuboresha na kuendeleza yale yote yaliyoanzishwa na serikali katika maeneo yao.
“Alichokofanya Mwenzetu mdau wa maendeleo Anania Mwigavile kimenigusa na kimegusa wengi naamini hiki alichokianzisha wengi tutafuata nyayo zake na naamini ipo siku na sisi mtaa wa Njeteni tutakuwa mfano katika mitaa yote katika jiji la Dar es salaam”,Amesema Godfrey Kayungi Mjumbe wa kamati ya siasa tawi la Njeteni.
Akizungumza kwa niaba ya Zahanati ya Kwembe kati Mwenyekiti wa Bodi ya Zahanati hiyo, Sikudhani Said amemshukuru mdau huyo wa maendeleo kwa kuwezesha uendelezaji wa eneo hilo la kuhudumia watoto huku akitoa rai kwa wadau wengine kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha eneo hilo linakamilika lakini pia miundombinu ya hospitali hiyo inaimarika.
“Kwa niaba ya zahanati nimshukuru Mkurugenzi wa Mount Zungwa kwa msaada alioutoa kwa ajili ya zahanati hii lakini niwaombe wadau wengine kuendelea kujitokeza ili kusaidia zahanati yetu sasa hivi watoto wabahudumiwa kwa kuchanganyika na wagonjwa wengine katika jengo moja lakini tukikamilisha eneo hili la watoto itasaidia watoto kupata huduma katika eneo lao,” amesema Sikudhani.