Home KITAIFA TAPSEA JIENDELEZENI KITAALUMA KUENDANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA- DK. BITEKO

TAPSEA JIENDELEZENI KITAALUMA KUENDANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA- DK. BITEKO

đź“ŚAwataka kuwa kielelezo cha huduma bora kwa wananchi

đź“ŚSerikali kufanyia kazi mapendekezo ya TAPSEA

đź“Ś Waraka wa muundo mpya wa makatibu mahsusi mbioni

Na Mwandishi wetu, Mwanza

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ametoa wito kwa makatibu mahsusi nchini kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia sambamba na kuboresha utendajikazi wao.

Ameyasema hayo leo Mei 23, 2024 Jijini Mwanza wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kumi na Moja wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi.

“Kama mnavyofahamu kuwa dunia ya leo ni kijiji kutokana na mabadiliko ya teknolojia na utandawazi ambayo kwa kiasi kikubwa unachochea maendeleo ya teknolojia hususan Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Ni jukumu lenu kama chama cha kitaaluma kuwa na mkakati wa kushawishiana kujiendeleza kitaaluma kwenda sambamba na mabadiliko ya TEHAMA. Dunia ya leo haitumii tena teknolojia ya “type writer” kama zamani ambavyo wachache wenu mliomo humu mlishatumia,” amesema Dk. Biteko.

“Mfumo wa kisasa wa matumizi ya kompyuta na vishikwambi ambao kwa pamoja unarahisisha utendaji kazi wenu, ni jukumu lenu kwa kada yenu waandishi waendesha ofisi kuhakikisha kuwa mnabobea katika fani hii na matumizi ya vifaa hivi kwenye kada yenu na hivyo ni muhimu mkafahamu matumuzi yake sahihi,”amefafanua.

Aidha, Dk. Biteko ametoa rai kwa makatibu mahsusi hao kutoa huduma bora kwa wateja wanaofika katika ofisi zao

“Fanyeni kila mmoja anayekuja ofisini kwenu atoke na furaha akiamini kuwa kodi anayolipa inamlipa mwenyewe katika kupata huduma bora, jinyimeni na kujizuia sana kuwa na kauli za kuvunja moyo kwa wateja wanaokuja kwenu na wakati wote mkiona miongoni mwenu mmoja wenu awe kwenye ofisi kubwa au ndogo mwenye tabia isiyofaa basi mkemeeni,”amesema.

Vilevile amewataka kusaidia wengine katika kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.

Dk. Biteko amesema kuwa Serikali itayafanyiakazi yale yote yaliyopendekezwa na TAPSEA.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema kuwa Serikali imefanya maboresho kadhaa katika kada ya makatibu mahsusi kwa lengo la kuboresha taaluma hiyo nchini.

“Awali taaluma hii ilikuwa inaitwa uhazili na kada yao hawa walikuwa wanaitwa makatibu mahsusi, tangu mwaka jana muundo umebadilika na sasa kwa kada yao wanaitwa waandishi waendesha ofisi na kiutumishi wamepanda kwa ngazi ya mshahara hadi kufikia TGSH. Hivyo ni maafisa hawa sasa wanasoma kufikia shahada hadi ngazi ya ubobevu,”amesema Simbachawene.

“ Wizara yangu ina jukumu la kuhakikisha inatoa waraka wa kuelezea majukumu haya mapya kwa waajiri ili nao wajue jambo hili,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania(TAPSEA), Zuhura Maganga amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kudumisha taaluma, kukuza uwajibikaji, kuipa hadhi taaluma yao, kuboresha maslahi yao pamoja na kutoa huduma bora kwa waajiri na wananchi.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya chama hicho kuwa ni kuishawishi Serikali kuanzisha shahada ya uhazili katika Chuo cha Uhazili Tabora na Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na kuboresha muundo wa maendeleo wa kada ya waandishi waendesha ofisi hadi kufikia daraja la afisa mwendesha ofisi mkuu.

Pamoja na mafanikio hayo, Zuhura ameiomba Serikali na waajiri nchini kuruhusu makatibu mahsusi kushiriki katika mikutano hiyo ya kitaaluma pamoja na kuwalipia ada za ushiriki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini (REA) imetoa fedha za kiasi cha shilingi bilioni 56 kwa ajili ya mradi wa usambazaji umeme vijijini na shilingi bilioni 12 kwa ajili ya mradi wa ujazilizi wa umeme. Hata hivyo kwa sasa mkoa huo unatumia kiasi cha megawati za umeme 73 ikilinganishwa na uzalishaji wa megawati 183.

Mkutano huo wenye kaulimbiu;“MAFANIKIO HUANZA NA UAMUZI BORA WA UTENDAJI, TUTUMIE MUDA VIZURI KWA KUFANYAKAZI NA KULETA TIJA” ulioanza Mei 20, 2024 umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 5000 kutoka mikoa yote nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here