Asema lengo ni kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini
Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya imedhamiria kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza kipato kwa wananchi wengi na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini.
Majaliwa ameyasema hayo leo Mei 23, 2024 kwenye ufunguzi wa Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji baina ya Uganda na Tanzania, katika Hoteli ya Johari Rotana jijini, Dar-es-Salaam.
“Ili kufikia lengo hilo, Serikali inatekeleza Mpangokazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini kwa kufanya mapitio na maboresho ya sera, sheria na kanuni ambazo zinakuwa ni kikwazo katika ufanyaji wa biashara nchini,”amesema.
Amesema Serikali imeimarisha utoaji huduma kwa kuunganisha mifumo ya kielektroniki 55 ya taasisi 50, pia sheria 13 zimeshafanyiwa marekebisho ili kupunguza au kuondoa kodi, ada na tozo na kupunguza au kuweka misamaha ya ushuru wa forodha.
“Mifumo hiyo imeunganishwa ili kubadilishana taarifa na kukamilisha uundaji wa mfumo wa kielektroniki wa dirisha moja la utoaji huduma kwa wawekezaji (Tanzania Electronic Investiment single window),”amesema.
Amesema mbali na maboresho ya mifumo, Serikali imeendelea kuimarisha nidhamu katika utendaji kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Pia amesema Serikali imeendelea kutoa ahueni za kikodi kwa wawekezaji katika viwanda vya ndani na kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara Tanzania (Blueprint Regulatory Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania).
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani kutoka sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili.
Majaliwa ameongeza kuwa jumla ya kampuni mpya 15 zenye mitaji ya Dola za Marekani milioni 215.48 zinazojishughulisha na uchakataji wa mazao ya kilimo na madini zimesajiliwa na kupewa leseni.
“Kutokana na jitihada mbalimbali, Serikali imewezesha uanzishaji wa viwanda 332 vya kimkakati na kurejesha viwanda 20 vilivyobinafsishwa. Tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua ya kugawa viwanda hivyo ambapo, EPZA wamepewa viwanda nane kwa ajili ya kuviendeleza, NDC na SIDO wamekabidhiwa viwanda viwili na viwanda kumi vilivyobaki bado vinatafutiwa wawekezaji wapya,”amesema.
Ametaja viwanda hivyo kuwa ni Mbeya Ceramics Company Ltd, Nachingwea Cashewnuts Processing Factory, Mafuta Ilulu Ltd, Mkata Sawmills Ltd, Tanganyika Packers Limited (TPL) Shinyanga Plant, Mwanza Tanneries Ltd, Mang’ula Mechanical and Machine Tools, National Steel Corporation, pamoja na Mbeya Meat Processing Plant.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa masuala ya uwekezaji na biashara watumieni makongamano hayo kubaini fursa za uwekezaji wa pamoja kati ya wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuweka bayana faida zinazotokana na uwekezaji wa pamoja.
“Ikiwezekana andaeni maonesho ya fursa hizi ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi zetu,”ameongeza.
Awali, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema wizara yao itaendelea kusimamia na kuratibu diplomasia ya uchumi kikamilifu na kwa uadilifu mkubwa ikiwa ni kutimiza ndoto na azma za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais Yoweri Kaguta Museveni za kukuza uchumi wa Tanzania na Uganda.
“Viongozi hawa wanataka biashara kati ya Tanzania na Uganda iongezeke maradufu na tukio hili ni utekelezaji wa ndoto na maelekezo hayo,”amesema.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Wizara ya Mambo ya Nje (Masuala ya Kikanda) wa Uganda John Mulimba amesema kuwa Tanzania na Uganda ni nchi rafiki zinazoshirikiana katika maeneo mengi yakiwemo ya kibiashara, kiusalama, kielimu, hivyo undugu huo ni chachu ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili ambao utasaidia kukuza uchumi wa wananchi wake kwa ujumla.