Home KITAIFA TMA YATOA TAHADHARI MWENENDO KIMBUNGA ” IALY KATIKA BAHARI YA HINDI

TMA YATOA TAHADHARI MWENENDO KIMBUNGA ” IALY KATIKA BAHARI YA HINDI

Na Mwandishi wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi. Kimbunga hicho kwa sasa kipo katika eneo la takriban kilomita 500 mashariki mwa pwani ya Dar es salaam.

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga “IALY” kinapungua nguvu yake huku kikielekea kaskazini, mbali na pwani ya nchi yetu na kinatarajiwa kuisha nguvu yake kabisa usiku wa kuamkia Mei, 222024.


Hata hivyo, kutokana na umbali kilipo kutoka nchini, vipindi vya upepo mkali vimeanza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani kama ilivyotabiriwa. Kwa mfano vituo vya hali ya hewa vilivyopo Unguja, Pemba na Mtwara vimeweza kuripoti upepo unaofika kilomita 50 kwa saa katika siku ya leo.

Matarajio ni kwamba, vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2 vitaendelea kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi yetu na katika Bahari ya Hindi kati ya leo tarehe 20 Mei 2024 na usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 22 Mei 2024 kabla kimbunga “IALY” hakijaisha nguvu yake kabisa.

Vilevile, Vipindi vya mvua vinaweza kujitokeza katika maeneo ya ukanda wa pwani (mikoa ya Tanga, Pwani (ikijumuisha Mafia), Dar es salaam, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) kati ya Jumanne tarehe 21 na Jumatano tarehe 22 Mei 2024.

USHAURI

Watumiaji wa bahari na wananchi wa maeneo ya ukanda wa pwani wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here