NaSaidina Msangi, Dodoma
SERIKALI imesema imeandaa Sheria na kanuni ili kumlinda mlaji, na kuhakikisha kuwa bei za bidhaa na huduma zinapangwa kwa msingi wa nguvu ya soko.
Hayo yameelezwa Mei 20 bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha. Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Mikumi, Dennis Lazaro Londo, aliyetaka kujua sababu za Wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za Kigeni wateja ambao ni raia wa Kigeni pamoja na athari zake.
Chande amesema kuwa biashara zimekuwa zikiendeshwa chini ya utaratibu wa soko huria ambapo bei za bidhaa na huduma hupangwa kuendana na uwiano wa uhitaji (demand) na upatikanaji wa bidhaa husika (supply), hata hivyo, wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.
‘‘Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini hivyo raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususan pale wanapokuwa na shilingi za Kitanzania,’’amesema Chande.
Amefafanua kuwa wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha havitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.
Ameeleza kuwa hakuna athari zozote za kimsingi za uchumi (economic fundamentals) kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa, kwa kuwa bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni.
Naye Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim Iddi, ameuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kurahisisha mfumo mzuri wa kutoa msamaha wa kodi kwa Wakandarasi wanaojenga barabara katika Halmashauri ya Msalala.
Akijibu swali hilo, Chande amesema kuwa Msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya Serikali unatolewa kwa mujibu wa kifungu cha Sita (6) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kama ilivyofanyiwa maboresho na Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021.
Amesema kuwa maboresho ya sheria hiyo yalilenga kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa msamaha wa kodi, ambapo awali mamlaka ya kutoa msamaha yalikuwa chini ya Waziri wa Fedha, na kwamba kwa mujibu wa marekebisho hayo, mamlaka ya kutoa msamaha yalikasimishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA.
‘‘Serikali kupitia TRA, ilianzisha Kitengo Maalumu kwa ajili ya kushughulikia misamaha ya kodi ya Ongezeko la Thamani ambapo kuanzishwa kwa Kitengo hicho kumesababisha kuwa na muda mfupi zaidi wa kushughulikia maombi ya msamaha wa kodi hiyo ukilinganishwa na wakati wa awali kabla ya maboresho,’’ amefafanua Chande.
Chande ameongeza kuwa katika jitihada za kuongeza ufanisi na kutoa msamaha wa kodi ndani ya muda mfupi, Serikali ilianzisha Mfumo wa Kieletroniki wa kuwasilisha maombi hayo TRA (Tax Exemption Mangement System).