Na Mwandisi wetu@Lajiji Digital
MKURUGENZI Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amewataka viongozi wa hospitali hiyo kutoa maamuzi na kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya usimamizi kwa wakati ili kuendelea kutoa huduma bora.
Profesa Janabi ametoa kauli hiyo Mei 21 wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Wakuu wa Majengo (Block Managers) yaliyoandaliwa na MNH kwa ushirikiano na Abbott fund kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao ili wakawajengee uwezo watumishi walio chini yao.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yataongeza chachu katika kuleta ufanisi katika kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwakuwa kila kiongozi atakuwa anajua wajibu wake ipasavyo na hivyo kutafsiri malengo ya taasisi kwa wale anaowaongoza.
“Wewe leo umepata mafunzo haya inabidi kila mmoja ajitazame na kujiwekea malengo ya watu ambao atawafundisha ambapo hata akiondoka Muhimbili aweze kujinasibu kwa kusema nimewafundisha watu kadhaa na leo wanafanya vizuri na sio kukaa na maarifa hayo mwenyewe,” amebainisha Profesa. Janabi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi Endelevu Abbott-Tanzania Dk. Festo Kuyandabila amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo ya uongozi ambapo mafunzo yanayofanyika leo yanalenga kuandaa wakufunzi ambao wataenda kufundisha watumishi wengine, ndio maana yamehusisha wakuu wa idara na wakuu wa majengo.
Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala MNH Chiku Wahady amesema mafunzo hayo ya siku moja yamehusisha viongozi takribani 54 wa Hospitali ya Taifa Mhimbili