Na Mwandishi wetu, Ukerewe
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Joshua Bituri Manumbu ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa jitihada endelevu za kuelimisha jamii namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko na kuwadhibiti pale wanapoonekana kuhatarisha maisha ya wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa Mei 08, 2024 na Mwenyekiti huyo katika ziara iliyofanywa na Maofisa wa TAWA wilayani humo.
“Tumekuwa na matukio mbalimbali ya mamba na viboko kujeruhi watu lakini kupitia elimu inayotolewa na Maofisa hawa wa TAWA na namna wanavyowadhibiti, wameweza kuokoa baadhi ya watu lakini pia wameweza kuwaondoa wale wanyama ambao wameshafikia hatua mbaya ya kudhuru watu,”amesema
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Maofisa wa TAWA kutoka Kanda Maalumu ya Mwanza na imetoa ushirikiano mkubwa kwa Maofisa hao ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Aidha amemshukuru Rais. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Maofisa hao vitendea kazi vinavyowafanya waweze kutekeleza majukumu yao kama sehemu ya taasisi muhimu nchini.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Selema kilochopo Kata ya Bwiro wilayani humo wameipongeza na kuishukuru TAWA kwa elimu wanayoendelea kuitoa wilayani humo ambayo wamekiri kuwa imekuwa msaada kwao na itawawezesha kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku wakiepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Selema wilayani humo, Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu serikali inahakikisha usalama wa mwananchi unakuwa ni kipaumbele cha kwanza na ndiyo maana mara kwa mara Maofisa wa TAWA wamekuwepo maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu na kufanya doria katika maeneo ambayo yanatajwa kuwa na changamoto ya wanyamapori hao.
Aidha Maganja ametoa wito kwa wananchi hao kuendelea kufanyia kazi maelekezo na elimu inayotolewa na wataalamu ili waendelee kuwa salama.