Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati kukaa pamoja na wadau ili kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa maboresho yatasaidia upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu nchini Tanzania.
Rais Dk.Samia ametoa agizo Mei, 8 hilo jijini Dar es Salaam wakati alipokua katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa taifa wa natumizi ya nishati safi ya kupikia, iliyofanyika katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha, amesema kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi nchini kuongeza uwekezaji na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia amewataka kuleta teknolojia rahisi itakayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao pamoja na kulipia kulingana na matumizi kama inavyofanyika katika umeme.
Amesema asilimia 90 ya watanzania bado wanatumia nishati ambayo sio rafiki, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamia utekelezaji wa mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia malengo asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi.
Vile vile amesema lengo la mkakati huo likitekelezwa na kutimia litapunguza gharama ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuongeza upatikanaji na uwekezaji wa nishati safi.
Amebainisha kuwa mkakati huo wa kitaifa pia utachangia jitihada za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa misitu ambao huchangiwa na shughuli za kibinadamu.
Amesema kwa sasa, inakadiriwa kuwa takribani hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka ambapo nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha kutoweka kwa misitu hiyo.
Awali akisoma taarifa ya Makakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amesema kuwa mradi huo utagharimu shilling trilioni 4.6 ambao utamudumu kwa muda wa miaka 10 mpaka 2034, huku akifafanua kuwa umefata sera za kitaifa na kimataifa ili kuleta tija.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo, amesema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya taifa ya nchi, huku akiadi utekelezaji kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa lengo la mikakati wa nishati safi ya kupikia ni kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania watumie nishati safi pamoja na kusimamia kikamilifu mkakati huo ili kuleta matokeo ya haraka na kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi