Na Mwandishi wetu, Magu
BARAZA la Madiwani wilayani Magu Mkoani Mwanza limekubaliana kugawa Jimbo la Magu kuwa Majimbo mawili kutokana na ukubwa wake wa kijografia ambao unafanya ugumu wa kuhudumia wananchi.
Hayo yamejitokeza Mei, 8 2024 wilayani humo katika kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka 2023/24.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Simon Mpandalume akizungumza kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri amesema kutokana na ukubwa wa wilaya hiyo yenye kata 25 wameona umefika muda kwa wilaya kugawanywa ili kurahisisha utendaji kazi.
“Sisi Balaza la Madiwani wa Halmashauri Wilaya ya Magu tunabariki kugawa jimbo la Magu ili kuwe na majimbo mawili kwani hicho ni kilio chetu cha muda mrefu,” amesema Mpandalume.
Amesema kuwa maendeleo yamekuwa hayafiki kwa wakati katika maeneo yote kutokana na jimbo hilo kuwa na Kata 25 hivyo ukubwa huo umekuwa unazorotesha maendeleo katika eneo hilo.
Naye Diwani wa Kata ya Bujora Bunyanya John amesema kugawa jimbo hilo Utarahisha huduma za maendeleo hivyo wanaomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassani kuona umuhimu wa kuwapatia jimbo jipya.