Na Esther Mnyika @@Lajiji Digital
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kuhakikisha mradi wa chuma wa Liganga unaanza uzalishaji na malighafi hiyo itumike kwenye viwanda vya hapa nchini.
Akizungumza leo Mei, 9, 2024 jijini Dar es Salaam, Dk. Samia wakati akizindua kiwanda cha kuunganisha malori na matipa cha Surtun kilichopo Kisarawe II Wilaya ya Kigamboni ambao umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali,Taasisi, Dini na wengine.
Amesema malighafi zinazopatikana katika mradi wa chuma wa Liganga utasaidia utengenezaji wa vipuri na bidhaa nyingine zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
“Mradi huu ni muhimu kwa uchumi wa viwanda vya chuma na mhakikishe mnapata mwekezaji mzuri atakayechimba chuma hiki na kisha kitumike kwenye viwanda vingine,”amesema Dk.Samia.
Amesema serikali itaendelea kujenga uchumi wa kisasa funganishi na jumuishi na shindani katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Amesema sekta ya viwanda inaongoza uzalishaji na kutoa ajira kwa wananchi jambo ambalo ni muhimu katika kukuza kusaidia katika mapambano ya kuondoa umaskini.
Dk. Samia amesema serikali imepunguza kodi ya makapuni kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 kwa kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ili kuchochea uwekezaji zaidi kwenye sekta ya viwanda.
“Kiwanda hiki ni chachu ya ukuaji wa viwanda na sekta nyingine kwa kuwa kutumia vioo vinavyozalishwa na kiwanda kingine ambacho zaidi ya asilimia 89 ya malighafi zake zinapatikana hapa nchini,”amesema.
Pia Dk. Samia amesema matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zinapunguza gharama kwa kampuni zenyewe zinazotengeneza magari na inaongeza manufaa ya uwepo wa kampuni hiyo kwa uchumi wa nchi.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira za moja kwa moja 250 na zisizo rasmi 1800 kuongeza mzunguko wa fedha, mapato ya serikali na kuimarisha teknolojia.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Dk.Ashatu Kijaji, amesema serikali imechukua uamuzi wa kulipa fidia wananchi wanaozunguka mradi wa madini ya vioo wa Engaruka uliopo Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Amesema malighafi zitakazopatikana katika mradi huo zitatosheleza kwa zaidi ya asilimia 99 ya viwanda vya vioo hapa nchini.
“Mradi huu ni muhimu kwa uchumi wa viwanda vya vioo na kwamba hakutakuwa na haja ya kuagiza malighafi nje ya nchi,”amesema Dk. Kijaji.
Amesema hatua hiyo ya serikali ni ushindi mkubwa kwa uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa za vioo hasa viwanda vilivyopo nchini.
Aidha amesema sekta ya viwanda imeajiri watu kutokana na kufanya marekebisho ya sheria, kanuni, miongozo kwa ajili ya wawekezaji.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mpango na Uwekezaji , Profesa Kitila Mkumbo amesema katika miaka mitatu iliyopita uchumi wa Tanzania umekua na kuimarika ukikua kwa asilimia sita
Amesema uchumi wa Tanzania umeimarika kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali katika kilimo na ujenzi wa miundombinu.
“Sekta ya viwanda imekuwa na mchango wa asilimia 10 katika miongo mitatu iliyopita lakini kwa sasa changamoto nyingi zimetatuliwa na ndio maana uwekezaji katika sekta hii unazidi kukua,”amesema Profesa Kitila.
Amesema kati miradi 526 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa mwaka jana, pekee na miradi 237 iliikuwa ni ya uzalishaji viwandani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Surtun Corporation Limited,Rehmtullah Habib amesema ni cha kuunganisha magari aina kuu mbili malori na matipa na kwa siku kuzalisha malori 30 na matipa tisa.
Amesema hadi sasa wamezalisha magari 150 na wanazalisha aina kuu mbili ambazo malori na matipa kwa ajili ya shughuli mbalimbali katika sekta ya ujenzi na madini.
” Kiwanda hiki kimeajiri watu 250 na ajirazisizo rasmi 1800 wakati tunaanza kuuza magari walikuwa 20 tangu kiwanda kianze ajira zimeongeza,”amesema Habib.
Aidha amesema bado wanahitaji kujenga kiwanda cha vipuri hivyo wameomba eneo la hekari 54 kwa ajili ya kiwanda hicho.