Home KITAIFA WAZIRI WA ULINZI AFANYA ZIARA KAMANDI YA JESHI LA AKIBA NA KULITAKA...

WAZIRI WA ULINZI AFANYA ZIARA KAMANDI YA JESHI LA AKIBA NA KULITAKA KUFANYA TATHMINI YA UTENDAJI TANGU KUANZISHWA KWAKE

Na Mwandishi wetu, Manyoni

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk.Stergomena Tax ameagiza Uongozi wa Kamandi ya Jeshi la Akiba kufanya tathmini itakayoainisha mafanikio, changamoto na kutoa mapendekezo yanayolenga kuliimarisha zaidi Jeshi hilo.

Akizungumza Mei, 7, 2024 Dk. Stergomena wakati wa ziara ya kikazi katika Kamandi ya Jeshi la Akiba, Mkiwa Manyoni amekumbushia umuhimu wa Jeshi la Akiba ambalo majukumu yake liliundwa kwa lengo la kuandaa nguvu ya akiba kwa ajili ya kusaidiana na Jeshi la kudumu JWTZ na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, kushiriki katika shughuli mbalimbali za Ulinzi wa nchi.

Amesema ikiwemo kushirikiana kuandaa na kufanya mazoezi ya Kijeshi, na kuandaa umma wa watanzania ili waweze kuelewa kuwa dhana ya ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila Mtanzania.

“Tunapo adhimisha miaka 60 ya JWTZ ni vyema na Kamandi ya Jeshi la Akiba ikatumia fursa hii kufanya tathmini ilipotoka na inapokwenda kwani Kamandi hii ni sehemu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Jeshi la Akiba limekuwa likishirikiana na mamlaka ya kiraia katika opereseheni mbalimbali na majukumu ya kitaifa, umuhimu wa Jeshi la Akiba unaonekana pia kupitia ushirikiano wake na mamlaka za kiraia hususan TAMISEMI ambao wamepewa jukumu la kuratibu mafunzo ya awali ya vijana katika mikoa na wilaya zote Tanzania Bara ambapo Kamandi hii hutoa wakufunzi kwa ajili ya mafunzo hayo,” amesema Dk.Stergomena.

Aidha amewapongeza pia Maafisa na Askari kwa kazi nzuri wanayoifanya katika utekelezaji wa majukumu yao na akawataka kuzingatia uwajibikaji kwa manufaa ya Taifa ili kuendelee kuliletea sifa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Akiba na Taifa kwa Ujumla.

“Yamekuwepo mafanikio mengi kuanzia ngazi ya Kata mpaka ngazi ya Kitaifa, baadhi ya mafanikio ambayo mmeyafanya ni kutoa mafunzo ya awali na kuwaongezea askari utayari, kushiriki katika mazoezi mbalimbali, kushiriki katika mazoezi ya medani na vikosi vya JWTZ, na kushiriki katika Ulinzi na Usalama katika maeneno ya Tanzania kwa kushirikina na mamlaka za kiraia, Ushiriki wa Jeshi la Akiba katika Vita ya Kagera mwaka 1979, kushiriki katika Opereseheni mbalimbali dhidi ya uhalifu na kushiriki katika opereseheni za uokoaji kama hivi karibuni katika maporomoko ya ardhi huko Hanang,” ameeleza.

Dk. Stergomena amesisitiza dhana ya Ulinzi wa Taifa kuwa ni jukumu la kila mwananchi kwa kunukuu moja ya kauli za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Haiwezekani Watanzania kuwa na Jeshi la kudumu kubwa lenye nguvu za kutosha kulinda mipaka mirefu ya nchi yetu bila kushirikiana kwa moyo mmoja na wananchi wenyewe huku akasisitiza Umuhimu wa ushirikiano baina ya Jeshi la Akiba na wananchi.

“Niwapongeze kwa dhati kwa kutimiza majukumu yenu ipasavyo na hivyo kuchangia katika kuimarisha ulinzi kuliletea Jeshi letu heshima, Wizara yetu na Taifa letu sifa kubwa, nitoe rai ya kuendelea kufanya vyema kwa weledi zaidi ili kuendelea kutunza heshima kwa Jeshi letu la Akiba na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetunza heshima ya JWTZ na heshima ya nchi yetu,”amesema.

Ameongeza kuwa Jamii yetu inatakiwa kuelewa mchango mkubwa wa Kamandi ya Jeshi la Akiba katika Ulinzi wa Taifa na kazi kubwa inayofanywa na Kamandi hii, kwani watu wengi hawajui mchango wake hivyo elimu ya kina inatakiwa kutolewa.

Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi ili kuongee na Maafisa na Askari, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Akiba, Brigedia Jenerali Erick Mlewa amesema kusudi la kuanzishwa kwa Kamandi hiyo ilikuwa ni kurahisisha uimarishaji, utawala na usimamizi wa shughuli za Jeshi la Akiba nchini.

Jeshi la Akiba lilianzishwa kwa sheria namba 2 ya mwaka 1965 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1966.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here