Home KITAIFA MWENGE WA UHURU 2024 WASHINDWA KUFIKA KWENYE MIRADI MIWILI RUFIJI, MAJI YAFUNIKA...

MWENGE WA UHURU 2024 WASHINDWA KUFIKA KWENYE MIRADI MIWILI RUFIJI, MAJI YAFUNIKA BARABARA

Na Mwandishi wetu, Rufiji

MWENGE wa Uhuru 2024 umelazimika kupokea taarifa ya miradi miwili ya maendeleo iliyopo Utete makao makuu ya wilaya ya Rufiji katika Kitongoji cha Bomba, kijiji cha Nyamwage baada ya Mwenge kushindwa kufika eneo la tukio kutokana na maji kufunika barabara.

Mbali ya msafara kukwama pia kijiko kilichokuwa kinategemewa kuvusha magari nacho kilinasa kwenye maji.

Miradi hiyo miwili ni kati ya nane iliyolengwa kutembelewa na kukagua ambayo ipo kata ya Utete kutokana na changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Miradi hiyo ni pamoja mradi wa barabara kiwango cha lami wenye thamani ya shilingi milioni 550 pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji kijiji cha Nyandakatundu, Utete wenye thamani ya shilingi milioni 7.9.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava akipokea taarifa ya miradi hiyo katika kitongoji cha Bomba Kijiji cha Nyamwage msafara ulipogeuzia, ametoa agizo la kuwasilishiwa kwa nyaraka na picha mjongefu (video ) Leo ili aweze kukagua miradi hiyo.

Awali akisoma taarifa ya mradi wa barabara ya Utete Meneja Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Rufiji, Hamisi Muhidini Chikaula amesema ,ujenzi ulianza kutekelezwa 11,agost 2022 na umekamilika April 10,2023 .

Ameeleza, mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 504.9 ikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu kupitia TARURA wilayani Rufiji na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100.

“Lengo la mradi huo ni kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha masuala ya usafirishaji,” anasema Chikaula.

Akizungumzia kuhusu mradi wa maji Kijiji cha Nyandakatundu ameeleza, ulianza kutekelezwa unatarajia kukamilika juni 1,2024 ambapo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 7.9.

Chikaula amefafanua, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 95 na utakapokamilika utahudumia wananchi 1,119 wa Kitongoji cha Nyandakatundu.

Kiongozi wa Wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa wa Mwaka 2024 Godfrey Mnzava amepongeza uongozi wa Wilaya ya hiyo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo sambamba na umakini wa usimamizi wa fedha zinazoletwa wilayani humo.

Aidha ametoa pole kwa wananchi walioathirika na mafuriko katika Wilaya hiyo ya Rufiji na kuwataka kuendelea kuchukua tafadhali kwa kusikiliza maagizo ya serikali kwa kuhama katika maeneo hatarishi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele akitoa taarifa wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2024 huko Umwe Kati wilayani Rufiji ukiwa unatokea wilaya ya Mkuranga amesema Miradi 7 itazinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru wilayani hiyo yenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 757 na kukimbizwa katika umbali wa kilomita 163.5 na miradi nane itakaguliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Ametaja miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ghala la chakula lililopo katika kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, bweni la wasichana shule ya Sekondari Ikwiriri, mradi wa mazingira katika shule ya msingi Shaurimoyo, shule ya msingi Mgomba kijiji cha Mgomba yenye watoto wenye uhitaji maalum na kutembelea kikundi cha ushonaji Umwe Kati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here