Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mafunzo kwa wataalam 52 kutoka Benki washirika kuhusu namna bora ya kutoa mikopo katika sekta ya kilimo pamoja na kuangalia viatarishi jambo ambalo litasaidia taasisi za fedha kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija kwa Taifa.
Akizungumza l Mei 3, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya wataalam ya kutoa mikopo katika sekta ya kilimo, Kaimu Mkurugenzi na Muendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dk. Kanael Nnko, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuleta tija katika utoaji wa mikopo sekta ya kilimo.
Amesema lengo ni kuhakikisha idadi kubwa ya wakulima wanafikiwa na kupata mikopo katika Mikoa yote kwa maendeleo ya Taifa.
“Tunaamini mafunzo haya pamoja na washiriki yanakwenda kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yetu na yatahakikisha sekta ya kilimo inasonga mbele,” amesema Dk. Nnko.
Amesema TADB katika kipindi cha miaka sita mpaka sasa mfuko wa dhamana ya Benki ya Kilimo imeweza kudhamini mikopo ya shilingi bilioni 270 kupitia benki washirika.
Ameeleza kuwa wameweza kuwafikia wakulima walengwa 24,000, huku benki ya washirika wametoa asilimia 11 ya mkopo katika sekta ya kilimo na kuendelea kuongeza juhudi ili kufikia mwaka 2030 sekta ya mikopo iwe imefika asilimia 30.
“Kilimo ni sekta kubwa hivyo huwezi kuwafikia wote kwa siku moja, juhudi zinaendelea kufanyika ili vijana, wakina mama na baba waweze kuingia katika sekta ya kilimo, ” amesema.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Ephraim Mwasanguti, amesema kuwa miongoni mwa majukumu yao ni kutoa elimu kwa mabenki na taasisi za fedha kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Amesema lengo la mafunzo ni kutoa elimu kwa maafisa wa mikopo ili waweze kutoa mikopo ambayo italipika na kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo.
“Tulipewa kazi na benki ya maendeleo ya kilimo ya kutengeneza programu kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo hasa ikilenga kuelimisha mabenki hasa maafisa mikopo ili waweze kutoa mikopo ambayo italipika kwa sababu hizi ni fedha za umma na kuleta matokeo mazuri katika nchi yetu,” amesema Dk. Mwasanguti.
Baadhi ya wahitimu wakiwemo Meneja Mahusiano Kitengo cha Wateja Wakubwa ABSA Benki, Mollen Charles pamoja na Meneja Uhusiano Kilimo Biashara Benki ya CRDB Salvatory Sylvester, wamesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia BoT Academy pamoja na washirika wengine kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) pamoja na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ambao wameshiriki katika kuunda mifumo pamoja na kufundisha lakini pia lengo likiwa kuzalisha wataalam wengi katika taasisi za fedha ambao watasaidia kutoa mikopo.