Home AFYA SIERRA LIONE WATEMBELEA JKCI KUJIFUNZA NAMNA WALIVOPIGA HATUA KUBWA KATIKA MATIBABU YA...

SIERRA LIONE WATEMBELEA JKCI KUJIFUNZA NAMNA WALIVOPIGA HATUA KUBWA KATIKA MATIBABU YA MOYO BARANI AFRIKA.

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

TIMU ya wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka Sierra Leone, wamefika nchini kujifunza namna ya kuanzisha matibabu ya moyo nchini kwao huku wakikagua uwekezaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kuingia makubaliano ya matibabu kwa kutibu wagonjwa kutoka nchini kwao kuja kutibiwa nchini.

Akizungumza Mei 3,2024 wakati akipokea ugeni huo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Piter Kisenge amesema ziara hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa matibabu ya moyo kati ya Tanzania na Sierra Lione ikiwa ni dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kutangaza tiba utalii nchini, ikiendelea kuzaa matunda.

“Timu hii imefika hapa nchini, kujifunza uwekezaji wa matibabu ya moyo na usambazaji wa madawa na vifaa tiba kutoka kwa Bohari ya Dawa (MSD), ikiwa ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Rais Dk. Samia,”amesema Dk. Kisenge.

Amesema timu hiyo ya wataalamu kutoka Sierra Lione imekiri kujifunza mambo mengi kutoka kwa JKCI, ambapo wataleta wagonjwa na wao kwenda kuanzisha taasisi yao kwa ushirikiano na taasisi hiyo.

Dk.Kisenge amesema wataalamu hao wa Sierra Lione, wamejifunza utendaji kazi mkubwa na imara kutoka kwa watumishi wa JKCI, ikiwemo namna ya kuhudumia wagonjwa.

Ameeleza kuwa, hatua hiyo ya kupokea ugeni huo ni hatua kubwa ambayo inatimiza malengo ya Rais Dk. Samia ya kukuza tiba utalii nchini.

Ameongeza kuwa, mbali na huduma za upasuaji wanazofanya hospitalini hapo, wanaendelea kutoa huduma za upimaji wa moyo kupitia mpango wao wa Dk. Samia Tiba Mkoba ambao unasogeza huduma hizo karibu na wananchi huku wakizijengea uwezo hospitali zingine za Kanda ikiwemo Benjamin Mkapa na zile za Chato na Geita.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Siera Lione, Sertie Kenneh, ambaye ni kiongozi wa msafara huo amesema, amefurahi kufika JKCI na kujifunza kazi kubwa ya matibabu ya moyo wanayoifanya kwa kuwa na uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba.

Ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa iliyofanya JKCI kwa kuwezesha matibabu ya magonjwa kwa wananchi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kuanzisha matibabu hayo.

“Tumejifunza vitu vingi namna ya utoaji huduma bora za matibabu kwa wagonjwa, ushirikiano uliopo baina ya watumishi wa taasisi ya JKCI kufanikisha lengo la huduma bora, hivyo nasisi tutaendelea kuimarisha ushirikiano,”amesema.

Amesema ubora wa huduma walizoziona JKCI watapeleka wagonjwa wao kutibiwa hapo ili kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa kwenda ulaya.

Naye, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI, Dk. Delila Kimambo, amesema mafanikio ya taasisi hiyo yanatokana na ushirikiano mkubwa walio nao watumishi wa Taasisi hiyo.

“Mafanikio haya yanayoonekana kwa ubora mkubwa katika kutoa matibabu sio ya jitihada za mtu mmoja, bali yanatokana na ushirikiano wa watumishi wote kuhakikisha tunafikia lengo lililokusudiwa,”amesema.

Amesema wataendelea kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali kuwavutia ili kuleta wagonjwa kutibiwa katika taasisi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here