Home KITAIFA DK. BITEKO APONGEZA MCHANGO WA KANISA KWENYE MAENDELEO YA TAIFA

DK. BITEKO APONGEZA MCHANGO WA KANISA KWENYE MAENDELEO YA TAIFA

đź“Ś Awahimiza Wachungaji kuwa na Maono Makubwa

đź“ŚAwataka kuhubiri amani na upendo

đź“Ś Awahimiza kumtia moyo Rais Samia kutekeleza miradi ya maendeleo

Na Mwandishi wetu, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewashauri wachungaji kuwa na maono makubwa katika kuongoza waumini katika makanisa yao ili kujenga Taifa la watu wenye mwelekeo chanya.

Akizungumza leo Mei 3, 2024 Jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao cha mazungativu (Retreat) kwa wachungaji wa Kanisa la FPCT, Dk. Biteko amesema ili waumini wapate uelekeo wa kwenda mahali fulani, wanahitaji mtu mmoja miongoni mwao atakaye waongoza kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na maono aliyonayo.

“Wachungaji msihangaike na wingi wa watu mahali popote, angalia uwezo wa kiongozi anayeona mbali atawaongoza wafike mbali.

“Askofu Mkuu umechagua fungu jema kufanya wachungaji hawa wakutane hapa kujiongezea maarifa kwa kuwa tuko katika dunia iliyojaa utandawazi na mafundisho ya kweli na yasiyo ya kweli. Ni vigumu kwa waumini kutambua ya kweli na yasiyo ya kweli hivyo, wanahitaji kuongozwa,”amesema Dk. Biteko

Aidha, Dk. Biteko amewahimiza viongozi wa dini kuwaongoza waumini kiroho na kuchagua viongozi sahihi wanaofahamu kuwa watawaletea maendeleo na ustawi wa nchi.

Pia, amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kufanya kazi kwa bidii, kuhubiri kuhusu amani pamoja na kusisitiza maadili kwa waumini.

Ametaja mafanikio mbalimbali ya Serikali inayoongozwa na Dk.Samia Suluhu Hassan, huku akiwaomba wachungaji hao kuendelea kumuombea na kumtia moyo ili aendelee kutekeleza miradi ya nchi katika maeneo mbalimbali.

“ Mradi wa reli ya kisasa (SGR) ni mradi mkubwa haikuwa rahisi kupata fedha za kutekeleza mradi huu lakini Rais Samia amefanikiwa, Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere unaozalisha megawati 2115 umefanikiwa, Pia Serikali imejenga madarasa, zahanati, vituo vya afya na kutoa ajira kwa watumishi wa sekta ya afya, angalieni nia yake, muungeni mkono”, amebainisha Dk. Biteko.

Vilevile, amesema serikali inatambua umuhimu wa dini na imani za watu hivyo viongozi wa dini wahimize waumini kuchagua viongozi wanaofaa

“Mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa dini mna uwezo wa kuwahamasisha waumini waweze kuchagua viongozi wanaowahitaji kwa ajili ya kuwaletea maendeleo,” amesisitiza.

Naye, Askofu Mkuu wa FPCT, Steven Mulenga amesema kuwa lengo la semina hiyo ya siku nne kwa wachungaji ni kuwajengea uwezo watumishi wa Mungu namna ya kumkaribisha Yesu Kristo.

“ Haya tuliyofundishana yatakuwa na matokeo kwa nchi ya Tanzania,”amesema Askofu Mulenga.

Semina hiyo wa wachungaji FPCT imehudhuriwa na wachungaji kutoka nchi za Kenya, DRC, Rwanda na Sudani Kusini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here