📌Awataka Watanzania kuwa waaminifu
📌Asisitiza ushiriki wa makampuni ya Kitanzania kuongezeka
📌Apongeza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kukuza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za kiuchumi
📌Atoa tuzo kwa makampuni yaliyofanya vizuri kwenye kuzingatia local content
Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kwenye uwekezaji miradi ya kimkakati kuhakikisha kuwa uwekezaji wanaoufanya unakuwa na tija kwa watanzania na kuongeza ushiriki wa watanzania kwenye kukuza uchumi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Aprili 27 jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa akifunga Kongamano la nne la Ushiriki wa Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji lenye lengo la kutoa maoni, kuimarisha ushiriki wa Tanzania kwenye mikakati mbalimbali na kuongeza ushiriki wake kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji.
” Rais amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha uwepo wa sheria ya local content kusaidia kulinda watanzania wanaofanya biashara lakini nataka niwaase pamoja na kuwa na sheria hii muhimu jambo la msingi ni kuhakikisha mswahili mwenzetu anapopewa kazi tumuunge mkono, tushirikiane nae ili miradi ya ndani iweze kwenda mbele,’’ amesema Dk. Biteko.
Aidha, amewataka watanzania kuhakikisha wanawaamini watanzania wenzao ambao wamepatiwa kazi na kuwataka kuifanya kwa uaminifu mkubwa ili kujijengea uaminifu na kuongeza kuwa wale wanaopata kazi kwenye miradi mikubwa wawe waaminifu hamna mtaji mkubwa duniani kama uaminifu.
Amesisitiza kuwa walipotoka kampuni ikija kuwekeza hapa nchini ilikuwa inaagiza kila kitu kutoka nje ya nchi na ndiomaana baraza limekuja na dhana ya local content ili kuipa nafasi nchi kuwa na nafasi kubwa ya biashara kufanywa hapa nchini na kufanywa na watanzania wenyewe kukuza uchumi
tufurahi kuona mswahili mwenzetu anapata kazi na kuifanya vizuri, waunge mkono washirikiane ili miradi ya ndani iweze kwenda mbele na kuifanya kwa uaminifu na kupunguza maneno, pambana na rushwa kwenye michakato, badala ya kutumia fedha hizo kuhonga na kupunguza mtaji pindi unapopata kazi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi watanzania wajaribu kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ile mikubwa ya kandarasi wasiwadharau waamini kuwa wanaweza, kwani hadi sasa ni takribani asilimia 97 ya miradi ya ndani imefanywa na watanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema kuwa kushirikisha wananchi kumiliki uchumi kwenye nchi yao kupitia dhana ya local content kunakwenda sambamba na mpango wa Maendeleo na dira ya nchi kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na hivyo kuinua uchumi wa nchi.
Amewashukuru washiriki wote kwa namna walivyojitoa kushiriki kongamano kwa kuhamasisha, kuhimiza na kujenga uelewa wa pamoja kuongeza ushiriki wa Tanzania kwenye masuala ya local content na hivyo kuleta Maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi, Bengi Issa amemshukuru Rais kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuongeza ajira, masoko na ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji.
Amesema watanzania wanapokuwa wanafahamu miradi inayoendelea kwenye nchi yao, watakuwa na ufahamu wa namna ya kujipanga kupitia kampuni zao na kushiriki kwenye michakato ya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sharia kanuni na taratibu kwenye utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya kiuchumi.
Awali Dk. Biteko alipata fursa ya kutoa tuzo kwa makampuni yaliyofanya vizuri kwenye nyanja za local content kwa upande wa uwekezaji pamoja na kutoa tuzo kwa wawekezaji, makampuni yaliyofanya vizuri ambapo kwa nyanja ya wawekezaji na wakandarasi wanaotekeleza local content imekwenda kwa kampuni ya bomba la mafuta ghafi la Afrika mashariki EACOP, Taasisi inayoshirikiana na baraza la uwezeshaji kiuchumi imekwenda kwa PURA.