Home KITAIFA ILINDENI TAALUMA YENU KWA WIVU MKUBWA – DK. BITEKO

ILINDENI TAALUMA YENU KWA WIVU MKUBWA – DK. BITEKO

📌Amevitaka vyombo vya habari kulinda maadili ya Mtanzania

📌Serikali kufanyiakazi madeni ya vyombo vya habari

📌Vyombo vya habari visaidie Serikali kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia

📌Serikali yafanya jitihada ya kupunguza gharama ya mitungi ya gesi

Na Mwandishi wetu, Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewataka Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuilinda taaluma ya habari kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi wa sekta hiyo nchini.

Ameyasema hayo leo Aprili 29, 2024 jijini Dodoma wakati akihutubia Jukwaa la Wahariri katika Mkutano wa 13 wa mwaka wa Kitaaluma uliohudhuriwa na Wahariri kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“ Watendeeni haki watu wanaokuwa vyanzo vyenu vya habari, mahali ambapo mnaona hawatoi ushirikiano tumieni mbinu mlizofundishwa kitaaluma ili kupata taarifa sahihi kutoka katika chanzo cha habari,”amesema Dk. Biteko.

Dk. Biteko amewataka Wahariri nchini kuhamasisha maudhui yenye maadili mema ili kufanya watanzania kujivunia utamaduni wao na maudhui yao, sambamba na kuwahamasisha wafanyekazi kwa bidii.

Pia, ametoa wito kwa Wahariri hao kuwakuza kitaaluma waandishi wa habari wachanga ili wafanye kazi kwa kuzingatia sheria, misingi na miongozo ya taaluma ya habari nchini.

Kuhusu madeni ya vyombo vya habari wanayodai katika Wizara, Taasisi na Mashirika ya Serikali, Dk. Biteko amesema “ Kuhusu madeni tutafanyiakazi jambo hili, Waziri nenda kaniandikie na tutatafuta namna ya kushughulikia ili wanaodai walipwe fedha zao,”amesema.

Aidha Biteko amesema kuwa Serikali itahakikisha matumizi ya gesi yanapewa kipaumbele na kuwa inafanya jitihada ili kupunguza gharama ya mitungi ya gesi kwa kushirikiana na wazalishaji pamoja na wasambazaji kwa kufungua vituo katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza gesi.

“Ifikapo mwaka 3034 tunataka asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, tunaomba ushirikiano wenu ili kufanikisha ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kasi kubwa zaidi na kama mnavyofahamu kuwa Rais Samia ni kinara wa uhamasishaji wa matumizi ya Nishati Safi ya kupikia hapa Barani Afrika,”amesisitiza Dk. Biteko.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali imeendelea kuboresha sekta ya habari nchini kwa kuimarisha uhuru wa habari ikiwa ni pamoja na kuanza kufanyiakazi teknolojia ya matumizi ya akili bandia nchini.

“ Tumewaambia wanahabari timizeni wajibu wenu, zingatieni sheria, taratibu na usawa,”amesema Nape.

Akizungumzia uundwaji wa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari amefafanua “Mchakato wa uundwaji wa taasisi hizi unaendelea na tayari uko katika hatua za juu ni imani yangu utakamilika na hivi vyombo vitafanyakazi,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile ameipongeza Serikali kwa kukutana na waandishi wa habari na kuelezea kuhusu utendaji wa shughuli zake.

Ambapo ameiomba Serikali kuongeza bajeti yake ya matangazo katika vyombo vya habari.

“Tunaomba bajeti ya matangazo iongezwe kwa kuwa Serikali ni mdau na mnufaika mkubwa kwa vile taarifa tunazoziandaa zinapelekwa kwa wananchi,”amesema Balile.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here