Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameainisha maeneo manne ya kimkakati Tanzania itakayoshirikiana na nchi ya Somalia ikiwemo katika masuala ya ulinzi na usalama wa raia.
Akizungumza Aprili 27 Ikulu jijini Dar es Salaam,na waandishi wa habari baada ya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mohamud Rais Dk. Samia amesema ziara yake ni ya kwanza nchini na kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo kufanya ziara tangu nchi hiyo iingie Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema katika mazungumzo aliyofanya na kiongozi huyo wa nchi hiyo ya Somalia wamegusia maeneo mbalimbali ya kimkakati yatakayosaidia kukuza uchumi wan chi hizo.
Amesema ziara ya Rais huyo iimeangalia namna ya kuboresha mahusiano kwa kuwezesha kuwepo na mfumo rasmi wa mahusiano.
“Tumeangalia namna ya kuboresha mahusiano kwa kuwa na mfumo rasmi wa mahusiano, tumekubaliana na mawaziri wetu wakutane wazungumze na kuibua maeneo ya kushirikiana,” amesema Dk. Samia
Aidha ameipongeza Somalia kwa kurejesha amani kwa nchi yao hivyo Tanzania itaendelea kuunga mkono katika jitihada za kurejesha amani nchini humo.
“Tumewaeleza utayari wa nchi yetu wa kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali ikiwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wa raia au maeneo mengine ya utumishi wa serikali.
“Tumewahakikishia kuwa tutaendelea kusisitiza umuhimu wa kuondolewa kwa zuio la ununuzi wa silaha kwa jeshi lao ambalo limewekwa kwao na itakuwa hatua ya kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama vya serikali na shirikisho la Somalia kutimiza wajibu wao au kujilinda wenyewe,” amesema.
Amesema hali ya Somalia haiko vizuri sana hivyo wamewahakikishia kuwaunga mkono katika kujenga uwezo wa wao kama nchi kujilinda wenyewe na serikali hiyo imekuwa ikichukua hatua kubwa ya kupongezwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Tumekubaliana kuimarisha mahusiano yetu ikiwemo ya kijamii hususani kwenye afya na elimu, tumewapa mwaliko wakati wote wakitaka msaada kwenye afya na elimu waje tuzungumze tupo tayari tutawasaidia.Tumewataka mawaziri wetu wakae wazungumze na kuyaona maeneo hayo,” amesema.
Rais Dk. Samia alimpongeza Rais huyo na nchi yake kwa hatua ya kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo Tanzania imeahidi ushirikiano katika kutekeleza masharti mbalimbali ya mtangamano ili manufaa ya hatua hiyo yawafikie Somalia na Tanzania.
“Mahusiano ndani ya mtangamano wa Jumuiya yetu yanawaweka watu mbele na kusukuma uhusiano wa kimasoko, hivyo tumezungumza nchi zetu mbili kuchukua hatua za makusudi kukuza biashara na uwekezaji kwa namna hiyo watu wetu wataweza kukuza fursa bora na mazingira bora ya ufanyaji biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema
Rais Dk. Samia ameahidi Rais Dk.Mohamud kuwa na ushirikiano katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ambazo nchi hizo ni wanachama.
Amesema mazungumzo waliyofanyana yametoa msukumo mpya wa kimahusiano hivyo mayumaini yake kuwa ziara hiyo itafungua milango mipya ya ushirikiano baina ya nchi hizo na kuwezesha serikali kuitumia vizuri fursa ya kiuchumi na kijamii zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
RAIS WA SOMALI
Akizungumza Rais wa Somalia,Dk. Mohamud amesema Tanzania wamekuwa washirika wa karibu ambao anahitaji waendelee kufanya nao kazi miaka ijayo na hiyo inatokana na misingi iliyopo ya kuheshimiana na kushirikiana katika maeneo mbalimbali.
“Ukweli Tanzania na Somalia tuna nguvu nyingi, nimefurahia majadiliano yetu kwa hakika tumeangalia maeneo mbalimbali ya kimkakati ya kuweza kutia nguvu zaidi mahusiano yetu, ninakuhakikishia kuwa yale yote serikali yetu imesema tutayafanya ili kudumisha ushirikiano huu kati ya nchi hizi mbili na kujenga mifumo mizuri ya kusaidiana kiuchumi tutayafanya,”amesema.