Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Natu Mwamba amewapongeza wafanyakazi wa wizara hiyo na Taasisi zake kwa kujisimamia vyema katika utekelezaji wa majukumu kwa kufuata miongozo ya Serikali na kuwataka kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miiko ya utumishi wa Umma.
Akizungumza Aprili 24 jijini Dar es Salam wakati akifungua Mkutano wa 37 wa mwaka 2023/2024 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha Dk. Mwamba amesema katika kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa fedha ni lazima kazi zifanywe kwa ubunifu na ushirikiano wa Wizara, idara, vitengo na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo nyeti na muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Amesema pamoja na kuwa wabunifu katika kazi zao na kujali usalama wa afya zao kwa kufanya mazoezi, kupata lishe bora pamoja na kupima afya zao.
“Niwapongeze kwa utendaji kazi wa Wizara ya Fedha na taasisi zake kupitia Government Structure inavyotekeleza majukumu yake sipati malalamiko ya moja kwa moja kuhusu Wizara yetu, Nawapongeza wakuu wa Taasisi na bodi za wakurugenzi na wafanyakazi kwa kujiendesha vyema chini ya bodi ya Wizara ya Fedha tupo vizuri taasisi zinajisimamia vizuri sana,” amefafanua.
Amesema baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu la majadiliano mahali pa kazi lililoundwa kwa mujibu wa sheria na kuipongeza Wizara hiyo kwa kutekeleza takwa hilo la kisheria la kuunda baraza la wafanyakazi ili kutoa fursa ya majadiliano ya masuala ya ajira na mazingira ya kazi baina ya mwajiri na mwajiriwa.
“Baraza la Wafanyakazi ni chombo muhimu cha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi muhimu yanayohusu uendeshaji na utendaji wa Wizara.Nasisitiza na kuelekeza kuwa ni lazima tuzingatie matakwa ya kisheria ya kufanya mkutano wa baraza la wafanyakazi na nipate taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya baraza kila tunapofanya mkutano kwa kuwa kupitia mikutano hii tukiwa taasisi nyeti tunapata fursa ya kuzungumza na kupanga mikakati bora ya kutoa huduma kwa wananchi na wadau wetu,” amesema.
Aidha amesema kuwa, Hoja zitakazojadiliwa katika mkutano huo zilenge kuboresha mazingira ya kazi, mifumo ya usimamizi na mpango wa Wizara na huduma kwa wadau wa ndani na nje.
“Katika kupiga hatua zaidi niwahakikishie kuwa Ofisi yangu ipo wazi kwa majadiliano ya hoja zote za kiutumishi, kiutawala na kiutendaji ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi na huduma kwa wadau wetu.Pia ni muhimu kuandaa programu za mafunzo ya masuala ya kitaaluma, kitaalam, maadili na umahiri mahala pa kazi na pia tuzingatie mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kutokea katika mifumo ya usimamizi wa fedha, mipango, uchumi, utawala bora na mazingira hii italeta chachu katika kutekeleza majukumu kwa weledi, ubunifu na uadilifu,” ameeleza.
Kuhusiana na suala la afya Dkt. Natu amewataka wajumbe wa mkutano huo kutekeleza majukumu yao bila kuathiri afya zao kwa kutenga muda kwa ajili ya mazoezi, kuzingatika lishe bora na kupima afya mara kwa mara kwa kuwa maisha ya utumishi bila magonjwa sugu inawezekana.
“Niwapongeze watumishi 301 wa Wizara ya Fedha waliojitokeza katika zoezi la uelimishaji na upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukiza mahali pa kazi Mwezi huu Aprili, watumishi 179 walikuwa wanawake sawa na asilimia 56.5 ya watumishi wote waliojitokeza na wanaume walikuwa asilimia 43.5 na watumishi hao walipata elimu na kupima sukari, msukumo wa damu, macho, afya ya akili na UKIMWI,” amesema.
Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa wengi wanakabiliwa na matumizi makubwa ya sukari, chumvi na mafuta kuliko mahitaji pamoja kutopata muda wa kupumzika hali inayopelekea wengi kuwa na uzito uliopitiliza na kuwashauri kuzingatia taratibu za afya wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Hazina,Scholastica Okudo amesema kuwa mkutano huo unafanyika kila mwaka kwa mujibu wa sheria na wizara imekuwa ikitumia fursa hiyo kukutana na kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi na wadau mbalimbali na kuchochea uchumi wa Taifa.
Amesema Wizara ya fedha imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa uwazi na utawala bora hali inapelekea utekelezaji wa urahisi katika kuziba mianya ya rushwa.
Katika mkutano huo wa siku mbili wajumbe hao watapata fursa ya kujadili mada mbalimbali ya Wizara hiyo ili kuendelea kuleta matokeo chanya kwa Taifa.