Home KIMATAIFA DK.BITEKO AMWAKILISHA RAIS SAMIA MAZISHI YA MKUU WA MAJESHI KENYA

DK.BITEKO AMWAKILISHA RAIS SAMIA MAZISHI YA MKUU WA MAJESHI KENYA

📌 Awataka wakenya kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu

📌 Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Jacob Mkunda ashiriki maziko hayo

Na Mwandishi wetu, Nairobi

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amemwakilisha Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwenye mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Kenya Jenerali Francis Omondi Ogolla, aliyefariki kwa ajali ya helikopta Aprili, 18, 2024 eneo la Kaben Marakwet Mashariki mwa Kenya.

Akitoa Aprili, 21 2024 salamu za Rais amesema kuwa, Dk.Samia anatoa pole kwa Rais wa Kenya, Dk. William Ruto, Wakenya na Familia ya marehemu Jenerali Ogolla na kuwaombea kwenye kipindi hiki kigumu.

“Mhe Rais amenituma niwape pole kwa msiba huu mkubwa hususani Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kumpoteza kiongozi makini, shupavu, wa ngazi ya juu na kuwaomba muwe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Dk. Biteko

Aidha, amewaasa Wakenya kuyaishi yale ambayo Jenerali Ogolla ameyaishi katika kipindi chote cha uhai wake, akiwa anawatumikia wananchi wa Kenya, na kuongeza kuwa yawe somo kwa wote hususani kwa vijana.

Rais wa Kenya,Dk. William Ruto amewataka Wakenya kuwa na subira katika kipindi hiki ambapo serikali imepoteza shujaa ambaye anatambuliwa kwa utendaji wake kama Mkuu wa Majeshi aliyeonyesha uwezo mkubwa katika utendaji kazi.

“Niwape pole Wakenya wote kwa msiba huu na niwaambie ningekuwa na uwezo wa kuchagua tena, ningemchagua Jenerali Ogolla kwani chini ya utendaji wake wa kazi, Jeshi la Kenya lilikuwa salama,”amesema Dk. Ruto.

Marehemu Jenerali Francis Omondi Ogolla alizaliwa Februari 12, 1962 katika Kaunti ya Siaya na alijiunga na jeshi la Kenya mwezi Mei 1984 na baadaye kutunukiwa cheo cha Luteni mwezi Mei 1985 ambapo alipangiwa kikosi cha Anga cha Moi na baadaye kupatiwa mafunzo ya Urubani.

Katika kipindi chote akiwa kwenye Jeshi la Kenya, Jenerali Ogolla alihudumu katika nyadhifa mbalimbali kwenye vikosi vya Anga hadi alipopandishwa cheo kuwa Jenerali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Kenya (CDF) Aprili, 28 2023.

Maziko hayo pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Kenya,Rigathe Gachagua, Waziri Mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) kutoka Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda, Spika wa Bunge la Kenya Moses Watengala Masika, wakuu wa vikosi vya majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Kenya, Malawi, Uganda Rwanda, Namibia, Burundi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here