Home KITAIFA SERIKALI KULIPA FIDIA ENEO LA IDEFU – MAKAMBAKO

SERIKALI KULIPA FIDIA ENEO LA IDEFU – MAKAMBAKO

Na Saidina Msangi, WF, Dodoma.

SERIKALI imesema kuwa imeanza taratibu za tathmini ya eneo la makaburi ya Idefu – Makambako na taratibu za malipo zitaanza baada ya kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

Hayo yameelezwa leo Aprili 19, 2024 bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha,  Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Makambako  Deo Kasenyenda Sanga, aliyetaka kujua ni lini Serikali italipa fidia eneo la Makaburi Idefu – Makambako ili kupisha ujenzi wa One Stop Centre.

Chande amesema  Serikali tayari imeshalipa fidia ya shilingi bilioni 4.6 kwa wananchi waliopisha eneo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa One Stop Centre.

Aidha, baada ya kupata majibu hayo Sanga ametaka kujua kama Serikali itaona umuhimu wa kulipa fidia hiyo haraka kwa kuwa kiasi kilichobakia si kikubwa, huku akitaka kujua wakati ambao Serikali italipa madai ya fidia kwa wananchi Kilolo waliopisha ujenzi wa makao makuu ya wilaya ambayo yameshawasilishwa muda mrefu.  

Chande amesema tayari Serikali imeshalipa fidia kiasi cha Shilingi bilioni 4.6 na kiasi kilicho baki ni milioni 100 na kumhakikishia Mbunge huyo kuwa ndani ya mwaka huu wa fedha Serikali italipa fidia iliyobakia.

‘‘Kwa upande wa Kilolo Serikali iko tayari kulipa fidia hizo haraka inasubiri Mthamini Mkuu wa Serikali atoe idhini ili malipo yaweze kufanyika,”amefafanua  Chande.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here