Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MKE wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Wanawake na kuwashirikisha katika ngazi ya maamuzi na kuendeleza maendeleo nchini.
Mama Mariam Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Uwezeshaji na Ushirikishwaji Wanawake kiuchumi kwa Zanzibar kupitia program ya Mwanamke Shujaa ilioandaliwa na kampuni ya Coca Cola Kwanza kwa kushirikiana na Oryx Gas Tanzania, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika viwanja vya Maisara , Mkoa wa Mjini Magharibi 20 Aprili, 20 2024.
Ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi inatambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na wajasiriamali Wanawake ikiwemo Mamalishe ambao ni kundi kubwa la Wanawake waliojiajiri kutoa huduma ya vyakula nchini.
Ametoa rai kwa mashirika na asasi mbalimbali za kiraia kuendeleza utaratibu wa ushirikishwaji na uwezeshaji Wanawake kiuchumi katika kufikia malengo ya maendeleo ya jamii .
Mariam Mwinyi amekabidhi majiko ya gesi 450 na mitungi yake, meza za majiko 450, kreti za soda 450 pamoja na Apron zaidi 1350 msaada uliotolewa na Kampuni ya Coca-Cola kwanza ikishirikiana na wadau wengine wa maendeleo wakiwemo Kampuni ya Oryx Energies , Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) pamoja na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).