Home KITAIFA POLISI KAGERA KUCHUNGUZA MAUAJI YA MWANAFUNZI ALIYEKUTWA AMEUWAWA KIKATILI.

POLISI KAGERA KUCHUNGUZA MAUAJI YA MWANAFUNZI ALIYEKUTWA AMEUWAWA KIKATILI.

Theophilida Felician, Kagera.

JESHI la polisi Mkoani Kagera linafanya uchunguzi wa kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka (11) mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya msingi Kilima.

Mwanafunzi huyo aliyetajwa kwa jina la Elius Antony mkazi wa kitongoji cha Ikande kijiji Kilima kata ya Nyakato Halmashauri ya Bukoba Mkoani Kagera alikutwa ameuwawa na kutelekezwa kichakani na mtu/watu ambao hawajajulikana.

Akitoa taarifa hiyo leo Aprili,15 2024 kwa kina kamanda wa jeshi la polisi Mkoa Kagera Ofisini kwake Manispaa ya Bukoba Blasius Chatanda hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kwamba tukio hilo linadaiwa kutokea mnamo Aprili,10 mwaka huu ambapo Aprili 11 majira ya saa 17:00 jioni alikutwa akiwa ameuwawa na mwili wake kutupwa kwenye pori la kijiji cha Kilima.

Kamanda huyo amefafanua kuwa mwili wa mtoto Elius ulikutwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya shingoni, sikio la upande wa kushoto na kichwani.

“Baada ya mtu au watu kutekeleza mauaji hayo walichukua mfuko wa sandarusi wenye rangi ya njano aliokuwa nao marehemu ukiwa na unga wa mahindi kilo mbili ndani yake, simu moja aina ya Tecno pp 2 pamoja na pesa shilingi 2500 ambayo ilibaki baada ya kulipa malipo ya kuchaji simu hiyo iliyokuwa chaji na matumizi mengine ya nyumbani,” amesema kamanda Chatanda.

Awali ameeleza kuwa kabla ya umauti kumkuta marehemu siku hiyo ya Aprili, 10 akiwa na baba yake Antony Kaloli umri miaka (42) wakiwa katika shughuli ya uchomaji mkaa baba yake majira ya saa 15:00 mchana katika kitongoji cha Mwizi alimtuma mwanaye huyo aende nyumbani kuchukua unga na simu hiyo ya Tecno katika sentre ya Mwizi alipokuwa ameiacha ikichajiwa dukani kwa Erneus Justinian hivyo baada ya kuchukua vitu vyote hivyo hakuweza kuonekana tena hadi alipokutwa ameuwawa.

Amesema kuwa baada ya jeshi hilo kupokea taarifa za tukio hilo lilianza uchunguzi ili kubaini niwatu gani waliohusika na unyama huo ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Mahakamani.

Ameongeza kwamba uchunguzi watukio hilo unaendelea vizuri hadi sasa, huku amesistiza kuwa wahusika wote watakamatwa kwa vyovyote vile.

Baada ya maelezo hayo ametoa onyo kali kwa wahalifu wote mkoani Kagera kusitisha mara moja vitendo hivyo kwani jeshi hilo litawasaka wale wote watakaoshiriki vitendo vya namna hiyo na waweze kushughulikiwa ipasavyo kwa mjibu wa sheria

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here