Home KITAIFA FCT YATOA MAFUNZO KWA WADAU

FCT YATOA MAFUNZO KWA WADAU

Na Mwandishi wetu, Arusha

BARAZA la Ushindani (FCT) limetoa mafunzo kwa Wadau Kuimarisha Soko Lenye usawa

Akifungua mafunzo hayo Aprili 9, 2024 jijini Arusha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha anayehusika na viwanda, biashara, na uwekezaji, Bw. Frank Mmbando, alipongeza juhudi za FCT katika kuimarisha ushindani wa haki na ulinzi wa watumiaji.

“Elimu hii ni muhimu sana kwa wadau wote katika Soko, itawezesha wadau kutambua haki na wajibu wao, kukuza ushindani wa haki, kuongeza uwajibikaji, na kutatua migogoro ya kiushindani kwa ufanisi,” amesema  Mmbando. 

Mmbando amehimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema elimu watakayoipata kutatua changamoto au migogoro ya kibiashara inayoweza kutokea kwa kuwa FCT ni chombo kinachosimamia haki kwa watu wote.

Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi FCT,  Kulwa Msogoti, ameongeza kuwa Baraza linahamasisha wadau wote wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, watoa huduma, na walaji ikiwemo jamii wawasilishe mashauri yao kwa  ngazi ya rufaa FCT endapo hawajaridhika na maamuzi yanayotolewa na Tume ya Ushindani na Mamlaka za Udhibiti za EWURA, LATRA, TCAA, TCRA na PURA.

Aidha, Msogoti amesema kuwa FCT inapokea, kusikiliza, na kutoa maamuzi ya rufaa yanayotokana na maamuzi ya vyombo hivi yanayohusiana na masuala ya ushindani wa kibiashara na udhibiti wa huduma mbalimbali kama vile maji, nishati, mawasiliano, usafiri wa nchi kavu na anga katika Soko.

Naye Afisa Sheria Mkuu wa FCT, Hafsa Said, amesisitiza kuwa FCT inatekeleza Sheria ya Ushindani, 2003 na Kanuni za Baraza la Ushindani za mwaka 2012 na Baraza linaweza kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka Sheria hii pamoja  na Sheria zilizoanzisha Mamlaka za Udhibiti tajwa hapo juu. 

Amesisitiza kuwa FCT ni Mamlaka ya mwisho katika Mfumo mzima wa ushindani wa kibiashara na udhibiti wa Soko ambapo mashauri yote ya rufaa yanasikilizwa.

Ameeleza utaratibu wa kushughulikia rufaa FCT,  Said, ameelezea kuwa Mtu anayekata rufaa analazimika kuwasilisha barua ya kuomba mwenendo wa shauri, nyaraka zote zilizosikilizwa mara ya kwanza  kutoka Tume ya Ushindani au Mamlaka za Udhibiti husika na sababu za rufaa na kuwasilisha mbele ya Baraza na kesi husikilizwa na kutolewa maamuzi ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita au kipindi kifupi kulingana na shauri lenyewe. 

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mdhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA),  Dismoso Chimbunde, amesema LATRA imeweka utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko kutoka kwa abiria kuhusu huduma za usafirishaji na iwapo hawataridhika na uamuzi wa LATRA, wanaweza kukata rufaa FCT ili  kuhakikisha ushindani wa haki.

Naye Mwenyekiti wa Daladala jiji la Arusha, Maulid Abdallah amesema elimu waliopewa na FCT imewasaidia kielewa kuwa wakipeleka malalamiko yao  LATRA wakiona wanashindwa kupata mwafaka au maamuzi yatakayowaridhisha watakata rufaa  FCT ili kupata suluhu ya kuendeleza  biashara zao.

Kwa upande wake  Kaimu Afisa Huduma kwa Wateja na Utawala EWURA CCC, Bi Sharifa Lengima   amesema elimu iliyotolewa na FCT  ni nzuri ili waweze kusaidia wateja  na amewashauri wateja kupata elimu katika huduma wanazotumia kwa kuwa Taasisi zipo kwa ajili ya kuwasaidia.

Baraza la Ushindani (FCT) limeandaa mafunzo kwa wadau wake wakiwemo wafanyabiashara, watoa huduma na walaji ikiwemo jamii kwa lengo la kuwaelimisha  kuhusu shughuli za Baraza la Ushindani na umuhimu wake katika Uchumi wa Soko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here