Home KITAIFA TUULINDE MUUNGANO NA TUUDUMISHE-DK.MWINYI

TUULINDE MUUNGANO NA TUUDUMISHE-DK.MWINYI

Na Mwandishi wetu,Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema ni wajibu kuulinda Muungano, kuuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi ili kuzidi kunufaika kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipofungua Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Maonesho ya Taasisi mbalimbali viwanja vya Nyamanzi , Mkoa wa Mjini Magharibi Aprili, 14 2024.

Ameeleza kuwa umoja wa Watanzania unazidi kuimarika , ushirikiano katika shughuli mbalimbali unaongezeka na amani inaendelea kudumu nchini.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano,”amesema Dk.Mwinyi.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka vipaumbele masuala ya kuimarisha Muungano.

Amesema Tanzania imefikia mafanikio makubwa kipindi cha Miaka 60 katika nyanja zote za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.

Rais Dk.Mwinyi amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki shamrashamra za sherehe za miaka 60 ya Muungano katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa ni pamoja na siku ya kilele Aprili, 26 2024 katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi mwaka 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo.

Aidha amesema Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na Duniani kote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here