Home KITAIFA MWENGE KUZINDUA MIRADI 8 YA MAENDELEO WILAYA TANGA

MWENGE KUZINDUA MIRADI 8 YA MAENDELEO WILAYA TANGA

Na Boniface Gideon, TANGA

MIRADI nane yenye zaidi ya shilingi bilioni 11 inatarajiwa kuzinduliwa na mwenge wa uhuru jijini Tanga Aprili 14, ambapo utakimbizwa kilometa 99.3, katika tarafa nne, kata 14 na mitaa 81 katika jiji hilo.

Mwenge wa Uhuru utahamasisha shuhuli mbalimbali za wananchi, ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini pia mapambano dhidi ya vvu, malaria, dawa za kuleya, rushwa pamoja na uhamasishaji wa lishe bora.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji akitoa taarifa ya ujio wa mbio za mwenge huo ofisini kwake, amesema mara baada ya mapokezi utakagua namna halmashauri hiyo inavyotunza mazingira na kudhibiti taka ngumu katika dampo la Mpirani na kupanda miti 50 ya matunda.

Amebainisha mwenge utafungua mradi wa maji mtaa wa Putuni wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2, lakini pia utakagua miti 300 iliyopandwa wakati wa mapokezi ya mwenge mwaka jana katika shule ya sekondari Kiomoni.

“Mwenge wa Uhuru utatembelea kituo cha watu wenye mahitaji maalumu cha YDCP kilichopo kata ya Central ambacho kilipewa wataalamu wanne na halmashauri ya jiji ikiwa ni juhudi za kushirikiana na wadau katika kuibua na kuwasaidia watu hao.

“Lakini pia utapokea taarifa ya halmashauri inavyopambana na dawa za kulevya pamoja na kutembelea shughuli za vijana ambao wamekopesha shilingi milioni 20 katika kituo cha kuoshea na ukarabati mdogo wa magari (Mkwakwani Youth Centre),” amesema Kaji.

Pia watazindua mradi wa ufuaji wa umeme wa jua kwenye kiwanda cha uzalishaji wa mifuko cha PPTL, wenye thamani ya shilingi bilioni 6.7.

Amesema kuna vyumba vinne vya madarasa katika shule ya msingi Majengo vyenye thamani ya milioni 100 vitafunguliwa, ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa ya lishe na mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI katika halmashauri hiyo.

Amesema vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi, shule ya msingi Mnyanjani vyenye thamani ya milioni 50 ambavyo ni mradi wa uliozinduliwa na mbio hizo mwaka 2023 vitakaguliwa.

“Kutafungualiwa klabu ya wapinga rushwa na dawa za kulevya katika shule hii pamoja na kupokea taarifa ya jinsi halmashauri inavyojiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa 20024,” amesema

Ameeleza kuwa mwenge utaweka jiwe la msingi katika zahanati ya Mzingani thamani yake ni milioni 150 na kupokea taarifa ya mapambano dhidi ya malaria.

Mwenge wa Uhuru utakagua barabara ya Askari na Lumumba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 ikiwa ni ukaguzi wa uendelevu wa miradi iliyowekewa jiwe la msinhi mwaka 2023, lakini pia utafungua barabara ya Jumbe na Dunia Hotel yenye urefu wa kilometa 1.2 yenye thaman ya milioni 817.

Vilevile utakapokea risala ya utii ya wananchi wa Halmashauri ya jiji kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na kukagua kongamano la vijana, pamoja na kukagua shuhuli za kijamii katika eneo la mkesha ambako ni uwanja wa shule ya sekondari Usagara.

Kaji ametoa wito kwa wakazi wote wa Wilaya ya Tanga kujitokeza kwa wingi katika mapokezi, katika njia utakapopita mwenge wa uhuru katika maeneo ya miradi na eneo la mkesha.

“Mkesha utafanyika katika shule ya sekondari ya Usagara, tumeandaa burudani ya kutosha, Mwenge ni faraja, tunataka hilo lionekane kweli, baada ya shuhuli nzima ya mchana, ikifika jioni wote tukutane pale tufurahi na kukesha na mwenge wet wa uhuru,”amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here