Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waumini wa dini ya kiislam kuendelea kuyaishi yale waliyojifunza wakati Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Ametoa wito huo leo Aprili 10, 2024 alipozungumza kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye swala ya Eid iliyofanyika katika msikiti wa Gadaffi jijini Dodoma.
Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha jamii inaendelea kuwa bora na kulifanya Taifa kuwa lenye tulivu, amani na mshikamano
“Popote Tanzania unapokwenda utulivu ni mkubwa kwasababu watu wake wanafuata misingi ya dini zao.
“Viongozi wetu wa dini Mwenyezi Mungu amewapa uwezo wa kuhudumia wanajamii na kuwaeleza yaliyomema, na wameendelea kutoa mchango kwenye Taifa hili ili liendelee kuwa na amani, Mwezi huu tumeona utulivu mkubwa, Mimi niwasihi utulivu huutuendelee nao katika kipindi chote cha miezi kumi na moja iliyobaki mpaka kufikia mwezi Mtukufu mwingine,”amesema Majaliwa.
Amesema kila mmoja anapaswa kufuata misingi iliyoimarishwa kwenye jamii zetu ikiwemo kupinga na kukataa ukatili dhidi ya watoto, wanawake na ulawiti
Amesema kuwa Rais Dk. Samia amekuwa mfano wa kuigwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani kwa kushiriki ibada ya futari na makundi mbalimbali katika jamii ambayo itawezesha kuijenga jamii yenye misingi imara
“Mwaka huu Rais wetu ametuongoza kwenda kwenye maeneo tofauti, tumemuona na watoto wadogo, wazee haya ni mafundisho makubwa yanayotokana na kiongozi wetu,”amesema
Majaliwa amewataka watanzania waendelee kuliombe Taifa ili liendelee kuwa na utulivu na amani.
“Utulivu wenu watanzania ndio mmefanya nchi hii iendelee kujiamini na kufanya kazi masaa yote bila shida, huu ndio utamaduni mzuri, tuendelee nao,”amesema.