Home KITAIFA BILIONI 96.47 KUONGEZA KASI YA MRADI WA UMEME WA KAKONO

BILIONI 96.47 KUONGEZA KASI YA MRADI WA UMEME WA KAKONO


Na Saidina Msangi, Dodoma.

SERIKALI ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa zimesaini mkataba wa Euro milioni 34.86 sawa na shilingi bilioni 96.47 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kakono.

Mkataba huo umesainiwa leo Aprili ni  9 2024 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-maamry Mwamba na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini Tanzania,  Celine Robert. 

Amasema mradi huo unaotarajia kukamilika mwaka 2026 na kukabidhiwa kwa Serikali mwaka 2028, utaongeza umeme wa megawati 87.8 kwenye gridi ya Taifa hivyo kuongeza uzalishaji wa umeme nafuu wa nguvu za maji ili kukabiliana na upungufu wa umeme katika gridi ya Taifa maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

‘’Mradi huu unafadhiliwa na Washirika watatu wa Maendeleo ambao ni AFD Euro 110 milioni sawa shilingi bilioni 304.37 Benki ya Maendeleo ya Afrika dola milioni 161.4 sawa shilingi bilioni 413.95 na Umoja wa Ulaya Euro milioni 34.86  sawa shilingi bilioni 96.47 kusimamiwa na AF ambayo tumesaini leo,” amesema Dk. Mwamba.

Amesema kuwa Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono unaenda sambamba na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) wenye kaulimbiu ya kujenga uchumi wa kiushindani na viwanda kwa maendeleo ya watu kwa kuboresha miundombinu yenye tija, upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha biashara na uwekezaji, mazingira wezeshi pamoja na mifumo ya elimu na mafunzo.

Amefafanua kuwa mbali na kusambaza umeme kwa watumiaji, mradi huo pia unatarajiwa kutoa fursa za ajira takribani 1,000 zitatolewa wakati wa awamu ya utekelezaji pamoja na ajira 100 za kudumu wakati wa awamu ya uendeshaji na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa watu wanaozunguka mradi na kuboresha Maisha yao.

Dkt. Mwamba ameishukuru AFD kwa jitihada zote za kuhakikisha kwamba, ruzuku hiyo inapatikana kwa ajili ya mradi na kuwa serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na AFD na washirika wengine wa maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa na kufikia lengo lililokusudiwa la maendeleo.

“Mradi huu unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya eneo hili linalokua kwa kasi, ambalo liko katikati mwa eneo la Maziwa Makuu, kukuza uchumi wa viwanda na kuchochea ukuaji sio tu Tanzania bali hata katika nchi jirani,” amesema  Robert.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema wizara hiyo kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) watahakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema mradi huo utarahisisha upatikaji wa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani, utaongeza ajira, utapunguza gharama za umeme na kuongeza mapato ya TANESCO.

Dk. Mataragio amelipongeza Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali huku akiitaja baadhi ya miradi ya nishati iliyofadhiliwa na shirika hilo ikiwemo Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu, Mradi wa kuungamisha Tanzania na Zambia pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua Mafia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here