Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote, Bara na Visiwani waendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ameyasema hayo leo Aprili 8, 2024 wakati akizindua nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. “Muungano huu ni tunu adimu na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Hivyo basi kila mmoja awe mlinzi.“
“Kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dk. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wao makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu,”amesema Majaliwa.
Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano yamebeba kaulimbiu isemayo, “Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,’ Tumeshikamana na Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa Letu’’.
Amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60.
“Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.
“Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla,”amesema.
Amesema kilele cha sherehe za muungano kitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia maadhimisho hayo.
“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu,“amesema.
Ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza.
Pia Waziri Mkuu amesema nchi itaendesha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, hivyo ametoa rai kwa wapigakura wote wahakikishe wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za kushiriki kuchagua viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na Muungano.
Aidha ametoa ratiba ya matukio yatakayofanyika kuwa ni pamoja na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano utakaofanyika Zanzibar tarehe 14 Aprili, 2024 pamoja na uzinduzi wa Maonesho ya Biashara ya Taasisi za Muungano. Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Amesema kutakuwa na Maonesho ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulla.
Majaliwa amesema kuwa Maadhimisho hayo yataambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo utakaoanza Aprili 15 na kuendelea hadi mwisho wa Mei, 2024.
“Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango ataliongoza Taifa katika siku maalum ya maombi na dua kwa Taifa itakayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili, 22 2024 Viongozi wa Kitaifa wa Dini zote watahudhuria katika ibada hiyo,”amesema.
Majaliwa amesema wilaya zote hapa nchini zitaandaa maombi kwa Taifa yatakayofanyika katika siku hiyo.
“Nisisitize kila Mkuu wa Wilaya aanze kufanya uratibu ili nchi yetu yote ishiriki katika maombi na dua hizo, ” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ataliongoza Taifa katika kuzindua kitabu cha Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais, shughuli itakayofanyika Aprili, 23 na 24, 2024 atatunuku Nishani za Taifa kwa watu mbalimbali, shughuli zote zitakafanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
” Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Muungano litakalofanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Jijini Dar es Salaam Aprili, 25 2024,” amesema
Waziri Mkuu amesema Aprili, 26 2024 Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ataliongoza Taifa katika kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano yatakayofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.