Home KITAIFA UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI NI WAJIBU WETU WOTE, TUUTEKELEZE IPASAVYO KATIKA MAZINGIRA...

UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI NI WAJIBU WETU WOTE, TUUTEKELEZE IPASAVYO KATIKA MAZINGIRA YOTE

📌Awasihi kuhakikisha wanakagua ubora wa viwango vya kazi zinazofanyika

📌Awasisitiza kulinda vifaa vinavyotoka stoo kufanya kazi iliyokusudiwa ili kupunguza upotevu wa fedha za shirika

📌 Ni mwendelezo wa ziara yake kukagua utendaji na kuwatembelea wafanyakazi kwenye maeneo yao

Na Amanda Tagame, Katavi

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amekutana na wafanyakazi wa Mkoa wa Katavi na kuwaasa kuhusu umuhimu wa kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi ya kuhudumia wananchi katika sekta ya nishati ya umeme kwani ni Shirika pekee lenye dhamana ya kutoa huduma hiyo nchini.

Ameyaeeleza hayo Aprili, 6 2024 katika kikao alichofanya katika mkoa wa Katavi akiwa katika ziara ya kukutana na wafanyakazi katika ofisi za TANESCO Kanda ya Magharibi.

Ameanza kwa kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Katavi pamoja na wafanyakazi wote kwa juhudi kubwa wanayoifanya licha ya kuwepo na changamoto nyingi katika mkoa huo lakini wamefanikiwa kufanya kazi nzuri. Amewaasa waendelee kuchapa kazi na kuhakikisha wateja wanahudimiwa katika viwango vizuri.

” Pamoja na changamoto zilizopo katika mkoa huu ikiwemo miundombinu mmeweza kupambana nazo niwapongeze na kuwashukuru na niwaombe muendelee zaidi ya hapo kutekeleza majukumu yenu,”ameeleza Mhandisi Gissima.

Ameongeza kuwa dhamana ya sekta ya nishati ya umeme iko kwa wafanyakazi wa TANESCO pekee nchini, ni wajibu wa kila mfanyakazi kuwajibika katika utendaji kazi wake ili kutimiza wajibu huo kikamilifu na kutoa huduma bora kwa Wananchi.

” Tumekabidhiwa jukumu la kuhakikisha umeme unapatikana tuhakikishe mida wote tunaweza kuwapatia wananchi umeme nchini,” amesema Mhandisi Gissima.

Amesisitiza juu ya kulinda na kutunza miundombinu ya umeme na kuwa ni jukumu la kila mfanyakazi kulinda mali za Shirika ili ziweze kutumika katika kuongeza ufanisi wa huduma. Amewataka viongozi kusimamia na kuhakikisha kazi zinazofanyika zinafanywa kwa viwango vinavyohitajika ili kupunguza uharibifu wa miundombinu ya umeme.

“Hakikisheni kuwa kazi zinazofanyika mnazikagua kuwa zimefikia viwango vinavyohitajika. Pia, hakikisheni vifaa vilivyotoka stoo vimefanya kazi iliyopangiwa kikamilifu ili kupunguza upotevu wa fedha za Shirika,” amesisitiza.

Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Katavi Mhandisi Seraphine Lyimo amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kutembelea Mkoa huo kuzungumza na wafanyakazi na kuahidi kusimamia maelekezo kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu mkubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here