Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo April, 5 2024 ameongoza baraza la biashara Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa Habari RC Chalamila amesema baraza hilo pamoja na mambo mengine limejadili uendelevu wa biashara za wazawa, sera za wawekezaji wa nje na wa ndani ya nchi
“Katika eneo hili malalamiko makubwa yamekuwa wageni kutoka mataifa ya nje kujihusisha na biashara za kichuhuzi katika eneo la karikoo ambazo zingeweza kufanywa na wazawa hivyo Serikali ya Mkoa inalifahamu hili na kinachotarajiwa kufanyika ni msako wa kawaida na kutoa elimu kuhusiana na jambo hili,”amesema Chalamila.
Vilevile baraza limejadili mfumo mzima wa biashara na mazingira yake, katika eneo hilo mjadala ulikuwa juu ya kufanya biashara saa 24 kwa kuwa tayari vyombo vya usafiri hususani mabasi ya mikoani yameshaanza kufanya kazi saa 24 hivyo iko haja ya biashara zingine katika mkoa kufanyika saa 24 ili kukuza uchumi wa nchi na Mkoa.
Chalamila amesema ili kufanya kazi saa 24 lazima kuwepo na ulinzi madhubuti, taa, pamoja na taasisi za fedha, hivyo mara Soko la karikoo likifunguliwa biashara katika eneo hilo zitafanyika saa 24 na maeneo mengine yatajifunza kutoka karikoo.
Vilevile baraza limejadili uchumi wa blue ambao unajikita katika uvuvi, usafirishaji, utalii, uzalishaji wa umeme, viwanda vinavyotumia malighafi za majini pamoja na mfumo mzima wa ajira.
Pia baraza limekubaliana kuweka nguvu sasa katika maeneo hayo ili kukuza uchumi wa Mkoa na Tanzania kwa ujumla na baraza limejadili faida za mkoa ulipo na mataifa mengine kwa maana ya Bandari hivyo ni vizuri kuwa na mikakati ya kutumia vizuri fursa zilizoko kwa masilahi mapana ya Taifa na Mkoa.
Chalamila amelihakikishia baraza kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, kuondoa urasimu kwa wakezaji kutoa ushirikiano wakati wote kwa sekta binafsi ili kwenda sambamba na maono ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.