Home KITAIFA MAJAJI, WASAJILI WA MAHAKAMA YA RUFANI WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA WA USIMAMIZI...

MAJAJI, WASAJILI WA MAHAKAMA YA RUFANI WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA WA USIMAMIZI MASHAURI.

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

JAJi  Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Majaji na Wasajili wa Mahakama ya Rufani nchini kuwa mstari wa mbele kuunga mkono matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Mhimili huo ikiwa ni pamoja na matumizi ya Mifumo yake hususani Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri kwa njia ya Ki-elektroniki (e-CMS).

Rai hiyo imetolewa  Aprili, 4 2024 jijini Dodoma na Jaji na Mlezi ‘Dean’ wa Mahakama ya Rufani (T),Augustine Mwarija kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania,  Profesa Ibrahim Hamis Juma wakati akifungua Mafunzo kwa Majaji na Wasajili wa Mahakama ya Rufani kuhusu Matumizi ya Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri kwa njia ya Ki-elektroniki (Electronic Case Management System e-CMS).

“Majaji wa Rufani chukueni nafasi yenu ya Uongozi katika matumizi ya Mfumo wa ‘e-CMS’. Mojawapo ya sifa ya Kiongozi bora ni yule anayeongoza mabadiliko ya kimaboresho na si yule anayebaki kusimuliwa kuhusu mabadiliko yanayoongozwa na wengine. Sina shaka, kwa kuwa Jaji wa Rufani kila mmoja anabeba sifa ya kiongozi bora na anapaswa kuongoza mabadiliko ya kimaboresho,” amesema Jaji Mkuu kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mwarija.

Amesema kuwa, matumizi ya Teknolojia ndio nyenzo ya karne ya 21 ya kuleta matokeo makubwa ya kusogeza huduma za haki zilizo bora, fanisi na wazi kuwa karibu zaidi na wananchi.

Kwa mujibu wa Profesa Juma amesema kuwa, Mfumo wa e-CMS ni injini wezeshi ya taratibu za kimahakama zilizokuwa zikitegemea watu na makaratasi huku akibainisha kuwa, Mfumo huo umezingatia taratibu za kimahakama ‘court business processes’ zilizopo na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za ujenzi wa mifumo.

Amesema kwamba, pamoja na faida ya haki kupatikana kutoka Mahakama ya Rufani kwa ufanisi, uwazi na kwa haraka, Mfumo wa e-CMS ni mfano hai wa Maboresho ya Mahakama yenye faida kubwa hapa kufanikisha ustawi wa wananchi wa Tanzania na Tanzania kwa ujumla.

Ameongeza kwa sasa, Mfumo wa e-CMS unaendelea kutumika na kuonyesha mafanikio makubwa katika ngazi za Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu na hivyo kuitaka Mahakama ya Rufani kujitayarisha kuutumia Mfumo huo kwakuwa muda si mrefu mashauri kutoka Mahakama Kuu yaliyopitia katika utaratibu wa Mfumo huo yatawafikia kwa maamuzi.

“Mahakama ya Rufani, tutaanza kutumia mfumo wa e-CMS katika kuwapangia Maombi (applications) yanayosikilizwa na Jaji mmoja mmoja wa Rufani. Baada ya kupata uzoefu na kufanyia kazi changamoto, mfumo utatumika katika mashauri yote ya Mahakama ya Rufani,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, ameeleza kuwa Mahakama za Nchi zote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na za Kusini mwa Afrika zimefikia hatua mbalimbali za kutumia e-CMS kuleta ufanisi na uwazi katika uendeshaji na usimamizi wa Mashauri.

Amewapongeza Maafisa TEHAMA na timu ya wajenzi wa Mifumo ya Mahakama kwa jitihada zao za kuendelea kutoa mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya wa ‘e-CMS’.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama ya Rufani (T),  Emmanuel Mrangu amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwapa mrejesho Majaji wa Mahakama hiyo kuhusu mafunzo yalitolewa mwaka jana yaliyohusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri.

Lengo la kikao hicho ni kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu maboresho yaliyofanyika kwenye Mfumo kufuatia mafunzo yaliyofanyika mwaka jana. Vilevile Wataaluma wetu wa Ujenzi wa Mfumo watawawezesha kufanya majaribio ya kutumia Mfumo kwa muda wa siku mbili,” amesema Mhe. Mrangu.

Mahakama ya Tanzania ilianza rasmi matumizi ya Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS)  Novemba, 6 2023 na kuacha kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (Judicial Statistical Dashboard System-JSDS 2) uliokuwa ukitumiwa awali ambao ulionekana kuelemewa na matumizi makubwa katika kusajili mashauri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here