Na Shomari Binda, Musoma
WACHEZAJI wa timu ya Biashara United wamesema zawadi pekee kwa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda ni kupanda ligi kuu.
David Kissu golikipa wa timu hiyo akizungumza na Lajiji Digital leo Aprili, 2 2024 amesema itakuwa zawadi bora kwa Rc Mtanda kama watapanda ligi kuu msimu huu.
Amesema mkuu huyo wa mkoa ambaye kwa sasa amehamishiwa mkoani Mwanza amekuwa chachu ya timu kufanya vizuri hadi sasa kwa nafasi walipo.
Kissu amesema amekuwa muhamasishaji katika kutafuta matokeo kwa kuwahamasisha viongozi na wadau wengine katika kila mchezo.
Amesema wao kama wachezaji wameahidi kujituma kwenye michezo iliyobaki ya Championship ili kuweza kushinda na kurejea ligi kuu.
Mchezaji huyo amesema hiyo itakuwa zawadi ya pekee kwa mkuu huyo wa mkoa kwa mazuri aliyoifanyia timu hiyo wakati akiwa mkoa wa Mara.
” Rc Mtanda amekuwa muhamasishaji namba moja ndani ya timu kwenye michezo yetu na kupelekea kufanya vizuri.
” Sisi kama wachezaji tumeahidi kupambana kwenye michezo iliyobaki ili zawadi yetu kwake iwe ni kurejea ligi kuu msimu ujao,” amesema Kissu.
Kwa upande wake Said Mtanda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara amewatakia kheri wachezaji na mashabiki wa timu hiyo katika michezo yao iliyobaki.