Home KITAIFA TARURA KAGERA YAFUNGUA BARABARA MPYA KM. 826

TARURA KAGERA YAFUNGUA BARABARA MPYA KM. 826

Na Mwandishi wetu, Kagera

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kufungua mtandao wa barabara mpya wa kilometa 826 katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na ongezeko la bajeti.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Kagera Mhandisi Avithi Theodory wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Theodory amesema kwamba TARURA imefanikiwa kufungua barabara hizo mpya ambazo awali zilikuwa ni changamoto kwa wananchi wa mkoa huo kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika eneo la huduma za jamii.

“Tumeweza kuwafungulia njia ambapo awali ilikuwa ni vikwazo kwa wananchi kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi kufikia huduma za kijamii, mfano mtu alikuwa akitembea Kilometa 21 lakini kwa sasa ni Kilometa 9, wapo wengine walitembea Kilomita 8 na sasa wanatembea Kilometa. 1.6 , hivyo tumejenga barabara mpya na sasa wananchi hawapati tena shida ya kutumia muda mrefu kufikia huduma za kijamii katika mkoa wetu,”Mhandisi Theodory.

Aidha, amesema Mkoa wa Kagera umetengewa bajeti ya fedha shilingi bilioni 31 mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka bilioni 9 kulinganisha na miaka ya nyuma, jambo ambalo limefanya barabara za mkoa wa Kagera za vijijini kufunguliwa kwa kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Kagera .

“Tangu Rais Dk. Samia aingie madarakani bajeti yetu imeweza kupanda mara tatu hadi kufikia bilioni 31 tofauti na bajeti ya awali na hivyo kufanya Barabara za mkoa wa Kagera hususani za vijijini kufunguliwa kwa Kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa huu,” ameongeza .

Pia amesema kuongezeka kwa bajeti hiyo imeweza kuongeza barabara zenye kiwango cha lami Kilometa 125 kulinganisha na Kilometa za awali, ujenzi wa makalavati 1,600 na kufanya maeneo mengi ya vijijini kupitika kwa urahisi na hivyo kuweza kusafirisha mazao yao kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine na kujipatia kipato.

Vilevile Serikali kupitia TARURA itaendelea kuhakikisha wanakuza miji kwa kuboresha miundombinu ya barabara ili wananchi wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara waweze kusafirisha na kuuza bidhaa zao nyakati zote katika masoko na katika kutekeleza hilo wamefanikiwa kufunga taa za barabarani zipatazo 240 na nyingine 140 zinaendelea kuwekwa sehemu mbalimbali katikati ya mji.

Naye Kudra Kagungu, mkazi wa Biharamulo amesema kuwa Serikali inapaswa kupongezwa kwa zawadi kubwa ya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na wananchi wanaondokana na kero katika matumizi ya Barabara mbaya hasa za vijijini.

Amesema uboreshaji wa barabara umeweza kuwasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja kwani hivi sasa maeneo mengi hakuna tena adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao kwani sehemu nyingi ambazo walitumia kiasi cha shilingi elfu 20,000 kufuata mzigo kwa Sasa wanatumia shilingi elfu 3,000 hadi 5,000 kwa sababu barabara zimeimarika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here