Na Mwandishi wetu, Same
MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amewataka Wananchi na Waumini wa dini ya Kikristo kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Mkuu huyo wa Wilaya ameyasema hayo Jana Wilayani humo wakati akizungumza na Waumini wa dini ya Kikristo kwenye ibada ya Pasaka Kanisa la T.A.G BATHEL REVIVAL TEMPLE.
Pia amewataka Waumini hao kutumia fursa hiyo ya ibada Pasaka kuendelea kuiombea nchi ambayo itaingia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni, lakini pia kuendelea kumwombea Rais wa Dk. Samia Suluhu Hassan, Mungu amlinde dhidi ya maadui wa nchi yetu na andelee kuliongoza vyema Taifa.
Vilevile, amewaomba Viongozi wa dini baada ya kumaliza kuongoza ibada kuwatangazia Waumini wote kujitokeza kwa Wingi kushuriki kuupokea Mwenge wa Uhuru ambao Kitaifa unatarajiwa kuzinduliwa Aprili 2 mwaka huu kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro na wao Wilaya ya Same wataupokea Aprili 8 pale shule ya Msingi Njoro ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.
“Shime shime Wananchi tujitokeze kwa wingi siku hiyo kuushangilia Mwenge wetu wa Uhuru, lakini pia niwakaribishe kwenye Mkesha wa Mwenge pale Shule ya Msingi Hedaru kutakuwa na mada mbalimbali kutoka kwa wataalam waliondaliwa bila kusahau burudani kutoka kwa wasanii nguri wa muziki wa Kizazi kipya,”amesema Mgeni.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu umebeba kauli mbiu isemayo “Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.