Na Mwandishi wetu,@Lajiji Digital
MWAKILISHI wa Afisa Maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam,Masalida Njashi amewatoa hofu mabinti wa Kata ya Kitunda Wilaya ya Ilala kuhakikisha wanajifunza masuala ya ujasiliamari kwa lengo la kujikwamua kiuchumia
Pia amelipongeza Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kuwekeza Wanawake na Mabinti la Ladies Joint Forum (LJF)kwa kushirikiana na Serikali katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali ambayo yanakuwa chachu ya kuwawezesha vijana kukua Kiuchumi kupitia mitaji midogo.
Akizungumza hayo leo Machi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Dada Kuoka yaliyoandaliwa na Taasisi ya LJF chini ya ufadhili wa Shirika la nchini Marekani la Marie – Schlei -Verein.
Amesema mafunzo hayo ya ujasiriamali kwa vijana yatatoa wigo mpana wa wao kujifunza mambo mbalimbali ya kuoka na kupika ili kuja kubadilisha maisha yao.
“Niwapongeze taasisi hii ya LJF kwa kuja kata ya Kitunda kuandilisha maisha ya Vijana wetu,pia niwapongeze wenyeviti wa mitaa kwa ushirikiano mzuri wanaowapa haya mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuwekeza nguvu kuwajenga vijana wetu.
“Mafunzo haya mtakayo yapata muyazingatie na muwe makini nayo msione kama mmekuja kutembea,kwani masuala ya Kuoka au Kupika hayajawai kukosa soko hivyo sio kitu kidogo mnachoenda kujifunza na ni kitu kikubwa sana,”amesema.
Amesema watu ujifunza mafunzo kama hayo kwa gharama kubwa hivyo vijana hao wamepata bahati ya kushiriki wanapaswa kuwa makini na kujifunza kwa ustadi mkubwa na kuja kuwa mabalozi wazuri wakuwaambia watu kwenye jamii kwamba kila kitu kinawezekana.
Naye Msajili wa Taasisi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,Aisha Ally amesema mradi huo una muda wa mwaka mmoja hivyo anaamini kuwa kipindi hicho chote watatoka wasichana wenye kuwa wapishi Bora.
“Nina imani katika kipindi cha mwaka mmoja tutakuwa tumepata wapishi wazuri sana kama tukizingatia yale tutayofundishwa na waalimu wetu,
Mafunzo ya kuoka yapo mengi na yanalipiwa kwa gharama kubwa lakini nyinyi mmepata nafasi ya kupata mafunzo haya bure hamgharamii chochote ,”amesema.
Amesema inawapasa vijana hao wa kike kujifunza kwa bidii na kutoka wakiwa na ujuzi wa hali ya juu.
Naye Mkurugenzi wa LJF ,Francisca Mboya amesema kuna umuhimu wa mabinti na wanawake kuendelea kuwezeshwa katika mafunzo mbalimbali ambayo yanawaletea wigo wa kujikwamua kiuchumi.
Amesema takribani wasichana 50 wa Kata ya Kitunda jijini Dar es Salaam wameweza kupatiwa mafunzo ya kujikwamua kiuchumi katika sekta ya upikaji wa vitafunio.
Amesema wameamua kuwawezesha mafunzo hayo wasichana wa kitunda kutokana na kupokea maombi mengi juu ya kuwawezesha wasichana katika sekta ya upishi wa vitafunwa.
Amesema wasichana hao kati walioanza kupatiwa mafunzo hayo ni kati ya umri wa miaka 18 hadi 40 ambapo watapitisha katika mada mbalimbali ikiwemo ya kuoka vitafunwa,Kuweza Kuanzisha Biashara zao na kujikuza kiuchumi.
Mboya amesema wasichana hao 50 wanatarajia kunufaika na mradi huo kwani wengi wao wametoka katika mazingira magumu hivyo LJF imeona ni vema kuwashika mkono na kuwasaidia.
”Mafunzo mengine tutakayowapatia ni uanzishaji wa biashara na kuongoza biashara zao na usawa wa kijinsia katika kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini huku wakiendelea kunufaika na kujipatia kipato.
”Awali tulikuwa na mradi huku kitunda kwa wasichana wa huku unaohusu Upiga Picha na tayari katika mradi huo tumefanya vizuri hadi sasa wasichana wapo katika kufanya kazi kwa vitendo,hivyo tuliona bado kunauhitaji wa kuja na kitu tofauti baada ya kupata maoni ya wadau wengi wa Kitunda,”amesema.
Amesema mradi huu utawasaidia vijana hao hata watakapokuwa na mtaji kidogo kuweza kujisimamia na kufanya vizuri katika kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mwalimu wa Mafunzo hayo ,Othman Ali amesema mafunzo hayo yataweza kuwajengea uelewa wasichana hao katika kupambana na ajira na kujiajili.
Amesema mwanafunzi atakapofunzu ataweza kujitegemea mwenyewe hata akipata mtaji kidogo.
Naye Mmoja wa wanufaikaji wa mradi huo , Mariam Nassoro amesema mafunzo haya yatamsaidia kwa kiasi kikubwa katika kujikimu kimaisha kwani mwanzo alikuwa hana ujuzi kamili wa kupika kama alivyopata mafunzo hayo.