Home KITAIFA RAIS DK. SAMIA AHIDI KUFANYIA KAZI RIPOTI YA CAG NA TAKUKURU.

RAIS DK. SAMIA AHIDI KUFANYIA KAZI RIPOTI YA CAG NA TAKUKURU.

Na Mwandishi wetu, Dodoma 

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amepokea Ripoti ya Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 na taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Akizungumza leo Machi 28 Ikulu Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa hizo, Rais Dk.Samia amesema ripoti hizo zinachangia maboresho na kuimarisha utendaji ndani ya serikali na mashirika ya umma.

Amesema dosari zilizotolewa zitafanyiwa kazi na kurekebisha ambapo mwakani hazitajirudia.

Samia ameongeza pia ripoti hizo zinasaidia kupunguza hasara ambapo mashirika mbalimbali licha ya kufanya kwa hasara yanakwenda mbele ukilinganisha na mwaka uliopita.

“Ongezeko la hati safi kwa asilimia 99 ambazo zinatokana na marekebisho ambayo hufanyika wakati Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali anatoa,”amesema Dk Samia.

Ameongeza kuwa ripoti hizo husaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya rushwa, kuimarisha nidhamu katika matumizi ya serikali na utendaji kazi.

Ameipongeza TAKUKURU mbinu ya kuibua kero kutoka kwa wananchi na kuzifikisha taasisi husika kufanyiwa kazi jambo ambalo linaifanya serikali kuwajibika ipasavyo.

Amempongeza CAG kuibua mambo na kupendekeza hatua za kuchukuliwa huku akihimiza utekelezaji uende kwa haraka.

“Kwa mujibu wa katiba, kazi yangu ni kupokea ripoti ya CAG lakini kazi yangu haijaisha, katiba inanitaka ninapozipokea ndani ya muda niwe nimezikabidhisha bungeni nami naahidi nitafanya hivyo,”amesema.

Akizungumzia kuhusu TAKUKURU, Rais Dk. Samia amesema taarifa za TAKUKURU zitafanyiwa kazi na maeneo yaliyoibuliwa yatafanyiwa kazi ipasavyo.

SALAMU ZA PASAKA

Rais Samia ametoa salamu za sikukuu ya Pasaka, kusherehekea sikukuu hiyo kwa usalama.

Awali Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akitoa matokeo ya ukaguzi wa ripoti za ukaguzi mwaka wa fedha 2022/23 amesema mwaka wa fedha 2022/23 alitoa hati 1209 za ukaguzi ambapo kati ya hizo hati 222 zinahusu tawala za Mikoa na mamlaka ya serikali za Mitaa, hati 215 zinahusu mashirika ya umma, 475 zinahusu serikali kuu zikihusisha hati 19 za vyama vya siasa na hati 299 zikihusisha miradi ya maendeleo.

Amesema kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni hati 1197 sawa naa asilimia 99, zenye shaka ni 9 sawa na asilimia 0.7, hati mbaya 1 sawa na asilimia 0.1 na hati mbili za kushindwa kutoa maoni sawa na asilimia 0.2.

Kichere amesema kwa ujumla hati za ukaguzi wa heasabu zinaonesha utayarishaji unaoridhisha wa hesabu unaozingatia kwa kiasi kikubwa taratibu na kanuni za uandaaji wa hesabu.

“Utayarishaji wa hesabu unazingatia viwango vinavyotakiwa vya kimataifa, “ amesema Kichele.

HALI YA UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA SIKU ZA NYUMA

Amesema katika ripoti za ukaguzi wa hesabu za miaka iliyopita, alitoa mapendekezo kadhaa yanayokusudia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuongeza tija katika uendeshaji wa shughuli za serikali.

“Natambua juhudi kubwa za serikali katika kufanyia kazi mapendekezo ninayotoa kwenye ripoti zangu za ukaguzi, pamoja na ofisi yako kutoa miongozo mbalimbali ya kushughulikia mapendekezo ya ripoti zangu,”amesema.

Amesisitiza kuwa mapendekezo hayo yatekelezwe kwa ukamilifu ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha na rasilimali zingine katika kutekeleza shughuli mbalimbali za serikali zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo.

DENI LA SERIKALI

Amesema hadi kufikia Juni 30, 2023 deni la serikali lilikuwa sh trilioni 82.25 sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka sh trilioni 71.31 kwa mwaka 2021/2022.

“Deni hilo linajumuisha deni la ndani la sh trilioni 28.92 na deni la nje la sh trilioni 53.32, kipimo cha deni la serikali kinachotumia pato la taifa kinaonesha kuwa deni hili ni himilivu,”amesema.

Amesema uwiano wa kulipa madeni na mauzo ya nje ni asilimia 12.7 chini kidogo ya kiwango cha ukomo cha asilimia 15 na uwiano wa  malipo ya madeni na mapato ni asilimia 14.3 chini kidogo ya kiwango cha ukomo elekezi cha asilimia 18.

USIMAMIZI WA MAPATO

Amesema ukaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), umebaini makusanyo ya shilingi trilioni 22.58 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 8 ukilinganisha na makusanyo ya sh trilioni 20.94 mwaka 2021/2022.

Amesema licha ya ongezeko hilo, makusanyo yalikua chini makusanyo yalikuwa chini kw ash trilioni 1.07 sawa na asilimia 4.5 ya makadirio.

Amesema licha ya mafanikio hayo, ukaguzi umebaini kuwa TRA  inakabiliwa na changamoto katika uthibiti wa bidhaa zinazopita nchini kuelekea nchi jirani kutokana na upungufu wa ving’amuzi vya kielektroniki.

“Upungufu huu unadhoofisha ufanisi katika kuhakikisha mizigo inayokwenda nje ya nchi kupitia mipaka yetu, mapungufu mengine yanayochelewesha utoaji mizigo kama ving’amuzi kukosekana kwenye mfumo , kuwa na taairfa zinazokosekana kwenye mfumo pamoja na kutowiana kwa taarifa kati ya vifaa saidizi na vifaa vikuu kwenye mfumo,”amesema.

Amependekeza serikali kufanya uchambuzi wa mara kwa mara wa upungufu wa mfumo wan a kupata ufumbuzi wake.

UKUSANYAJI MAPATO USIOKUWA WA KODI

Amesema alibaini mashirika 8 ya umma yalikusanya mapato ya sh bilioni 23.27 nje ya mfumo wa kielekroniki ya mfumo wa serikali (GEPG) kinyume cha waraka wa hazina namba 3 wa mwaka 2017.

Amesema kushindwa kukusanya mapato kupitia mfumo huo, kunaweza kusababisha upotevu wa mapato kudhoofisha juhudi za udhibiti na uwazi katika mapato ya serikali.

Amesema mapato yasiyokusanywa ya shilingi bilioni 61.15 na mapato yasiyowasilishwa benki ya sh bilioni 6.19.

Amsema ukaguzi umebaini kuwa Halmshauri zilizokusanya shilingi bilioni 61.15 kutoka katika vyanzo muhimu na vikubwa wakati shilingi bilioni 6.19 zilizokusanywa hazikuwasilishwa benki.

“Hali hii inaathiri uwezo wa Mamlaka za serikali za mitaa kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa jamii,”amesema.

MAPATO YA NDANI AMBAYO HAYAKUTENGWA KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO NA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA VIJIJI AU MITAA SH BILIONI 20.23.

Amesema Mamlaka 184 za serikali za mitaa hazikutenga shilingi bilioni 20.23 za mapato ya ndani iwa ajili ya miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji.

“Hii inajumuisha shilingi bilioni 17.60 za miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 2.63 zilizotakiwa kutumika kwa shughuli za uendeshaji wa vijiji , mitaa, Kilimo, uvuvi, ufugai na ufadhili wa miundombinu ya barabara kupitia Tarura.

Amependekeza Mamlaka ya serikali za mitaa kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kutenga mapato ya ndani kama ilivyohitajika na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

USIMAMIZI WA MATUMIZI

Amesema ukaguzi ulibaini kuwa Bohari ya Dawa (MSD) imetoa vifaa vya maabara vya upimaji Covid 19, ambapo kampuni iliyopewa kazi hiyo haikuwa watengenezaji wa vifaa hivyo kinyume na masharti ya zabuni.

“MSD ilinunua vifaa kutoka kampuni hiyo bila ushauri wa kiufundi wakutosha, baada ya vifaa hivyo kufika wataalamu waligundua kuwa havifai kwa mashine zetu hata hivyo MSD ililipa fedha zote,”amesema.

Kichere amependekeza wafanyakazi kuchukuliwa hatua kwa kurudisha fedha hizo za umma.

UTARATIBU DUNI KATIKA KUTEKELEZA MIRADI

Amesema jitihada za serikali katika ujenzi wa barabara zinakwamishwa na utaratibu duni kati ya taasisi za serikali hali inayosababisha ucheleweshaji, upotevu wa fedha na kuathiri ujenzi wa miundombinu muhimu kwa wananchi.

Ametaja taasisi hizo kama Shirika la umeme Tanzania(TANESCO), na Mamlaka za maji kuingilia miradi ya barabara inayosimamiwa na Tarura.

USIMAMIZI WA MIKATABA

Akizungumzia kuhusu malipo ya riba na kuchelewesha malipo ya wakandarasi, amesema ukaguzi umebaini matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma katika taasisi mbalimbali za serikali yanayosababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 222.34.

Amesema hasara hiyo inatokana na kucheleweshwa kwa malipo kwa wakandarasi wa miradi ya barabara na kusababisha malipo makubwa ya riba.

Amependekeza serikali kuandaa mpango Madhubuti utakaowezesha kufanya malipo ya wakandarasi kwa wakati kama inavyobainishwa kwenye mikataba ili kuepusha riba.

“Nashauri serikali iangalie uwezekano wa kupunguza miradi mipya ya barabara na badala yake imalizie iliyopo ili kupunguza malipo yanayotokana na riba,”amesema.

MITA ZA UMEME KUBADILISHWA KABLA YA MUDA

“Mita 10,8088 za umeme za TANESCO kati ya mita 60,2269 zilibadilishwa na TANESCO kabla ya kipindi cha uhai wa matumizi yake kuisha, kati ya mita hizo mita 13,493 zilibadilishwa ndani ya mwaka mmoja baada ya kufungwa kwake na mita 90,595 zilikuwa na muda mfupi wa matumizi kati ya mwaka mmoja na miaka 15 kinyume na muda unaokubalika kwa miaka 20 kwa mujibu wa TANESCO wenyewe.

“Kubadilisha mita mapema kunasababisha gharama kubwa kwa TANESCO napendekez Wizara ya Nishati ichunguze sababu ya TANESCO kubadilisha mita mapema pia Wizara ihakikishe vipimo vya ubora wa mita vinafanyika ili kuongeza ufanisi wa mita,”amesema. 

MASHIRIKA YA UMMA YANAYOJIENDESHA KIBIASHARA KUPATA HASARA 

 Kichere amesema Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), katika mwaka wa fedha 2022/2023 imepata hasara ya shilingi bilioni 56. 64 sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya sh. bilioni 35.24 iliyoripotiwa mwaka uliopita.

Amesema anatambua kuwa hatua mbalimbali ambazo Serikali ya awamu ya sita inazichukua ili kuwezesha kampuni hiyo kujiendesha kwa faida, ikiwemo kuundwa kwa Timu ya Wataalamu inayofanya tathmini ya masuala ya kiufundi, kifedha na utendaji wa ATCL katika biashara ya usafiri wa anga ili kuishauri Serikali hatua sahihi za kuchukua.

“Hata hivyo katika mwaka wa fedha 2022/2023 kampuni hii imepata hasara ya shilingi. bilioni 56. 64 sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya shilingi bilioni 35.24 iliyoripotiwa mwaka uliopita, kampuni imetengeneza hasara hii licha ya kupokea ruzuku ya shilingi bilioni 31.55 kutoka Serikalini na kuonesha shilingi bilioni 9.71 ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023,”amesema.

Akizungumzia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), amesema mwaka kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Shirika limepata hasara ya sh. milioni 894.

Amesema hasara hiyo imepungua kwa asilimia 94 ukilinganisha na hasara ya shilingi bilioni 19. 23 ambapo Shirika limetengeneza hasara hiyo licha ya kupokea ruzuku ya shilingi bilioni 4.55 kutoka Serikalini na kuonesha shilingi bilioni 4.4 ikiwa ni ya sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, limepata hasara ya shilingi bilioni 100.70 ambayo aimepungua kwa silimia 47.32 ukilinganisha na hasara ya shilingi bilioni 190.01

“Hata hivyo hasara hii imetokea licha ya kupokea ruzuku ya Tsh. bilioni 32.81 kutoka Serikalini kwa ajili ya matumizi ya kawaida sio matumizi ya maendeleo,”amesema.

Awali Mkurungenzi waTaasisi ya Kuzuia na Kupambana an Rushwa (TAKUKURU), Salum Hamduni akitoa ripoti amesema mwaka wa fedha 2022/2023 taasisi hiyo imebaini viashiria vya rushwa kwenye miradi ya maendeleo 1800 yenye thamani trilioni 7.7.

Amesema miradi waliyoangalia ni ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko Jiji la Dodoma, mradi wa maendeleo unaotelelezwa kwa kutumia njia ya forced account kwenye Halamshauri ya Jiji la Arusha,mradi wa ujenzi wa soko la wamachinga katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Pia walifuatilia miradi 12 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye thamani ya sh bil 107.4 katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Tabora na Mbeya.

Amesema matokeo ya ufuatiliaji yalionesha uwepo wa mianya ya rushwa ambapo baadhi ya miradi ilionekana kutosajiliwa na bodi ya usajili ya wakandarasi, wakala wa usalama mahala pa kazi, ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha uwepo wa riba.

“Malipo hufanyika pasipo baadhi ya kazi kufanyika, malighafi za ujenzi kutopimwa ubora wake kinyume na mikataba, ujenzi kufanyika kinyume na matakwa ya mkataba, kutozingatiwa kwa sheria na kanuni za ununuzi wa umma, kuwepo kwa nyongeza ya kazi pasipo kufuata utaratibu,”amesema.

Amesema kutokana na matokeo ya ufuatiliaji, takukuru ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo marekebisho husika yanafanyika ili kuhakikisha serikali haipati hasara.

Ameongeza kuwa walitoa ushauri wa miradi, kushauri mamlaka husika namna bora ya kuziba mianya ya rushwa ambayo ilibainika.

Amesema katika ufuatiliaji wa miradi 1800, miradi  171 yenye thamani ya shilingi bilioni 143,3 ilibainika kuwa na utekelezaji hafifu ambapo uchunguzi ulianzishwa.

Amefafanua kuwa miradi hiyo ilikua katika sekta ya ujenzi, fedha, maji, kilimo pamoja na majengo.

Hamduni amesema walitoa mapendekezo 3668 yalitolewa ili kurekebisha kasoro zilizobainika katika ufuatiliaji huo na kuhakikisha marekebisho kwenye miradi husika yanafanyika kwa gharama za mkandarasi au fedha inarudishwa serikalini.

“Mapendekezo 2740 yalitekelezwa sawa na sawa na asilimia 89.4 ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na takukuru,”amesema.

Amesema TAKUKURU ilifanya kazi ya uchambuzi wa mifumo 790 ya utoaji wa huduma kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa iliyobainika ikiwemo tathmini ya matumizi ya force account katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.

Amesema tathmini hiyo ilifanyika kutokana an kuwepo kwa changamoto ya utekelezaji wa miradi kwa njia ya forced account ambapo baadhi ya miradi iliyotekelezwa ilikuwa chini ya kiwango, gharama kubwa na kutozingatiwa taratibu za ununuzi.

Amesema kwa ujumla uchambuzi ulibaini baadhi ya watendaji waliokuwa wakisimamia miradi kwa kutumia force account kutokuwa na uelewa au kuwa na uelewa mdogo kuhusu taratibu za manunuzi, ukiukwaji wa sheria na miongozo wakati wa kuunda kamati za usimamizi, ukiukwaji wa sheria wa usimamizi, kutokuwepo kwa mfumo wa udhibiti wa ueledi na taaluma katika utekelezaji wa miradi inayotumia force account.

Pia upungufu wa wataalamu, ukosefu wa fedha za usimamizi wa muda wa utekeelzaji wa miradi, kutokuwepo kwa ukomo wa matumizi ya force account.     

Amesema walifanya uchambuzi wa mfumo wa uzingatiaji wa taratibu za ujenzi wa vituo vya mafuta katika  Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, uliohusisha vituo vya mafuta 38 na kubaini asilimia 79 ya vituo hivyo kuzingatia sheria ya kuwa na vibaki vya ujenzi kutoka katika Halmashauri ambapo uwekezaji umefanyika.

Amesema asilimia 21 ya vituo vilivyofikiwa havikuwa na leseni wakati wa ufuatiliaji ukifanyika, kuwepo kwa maombi ya ubadilishwaji wa matumizi ya ardhi kutoka yaliyokuwa yamepangwa na kuwa vituo vya mafuta.

Hamduni ameongeza ujenzi wa vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu kuongezeka na kuleta hofu ya usalama kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo,

Amesema katika kuzuia vitendo vya rushwa, takukuru ilibuni takukuru Rafiki inayohusisja mikutano ya wanufaika huduma inayotambua kero katika uitoaji wa huduma au katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo kama hatua hazitachukuliwa zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa, manung’uniko katika ngazi hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here