Na Mwandishi wetu, @Lajiji Digital
Umoja wa Wanawake Nchini(UWT) umedhamiria kwa vitendo kuhakikisha unatekeleza dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inamtua kuni mwanamke kichwani kwa kuhakikisha inazalisha nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.
Hayo yamesemwa leo Machi 28, Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa UWT Joketi Mwegelo baada ya kufanya mazungumzo na a wawekezaji kutoka nchini China katika jimbo la Changzho walioletwa nchini na kampuni ya Amec Group kwa kushirikiana na Canopus Energy Solution.
Amesema lengo la ugeni huo ni kujadiliana na kuangalia wanaweza kushirikiana kwenye maeneo gani katika uwekezaji wamekuja wakati muafaka kwani Chama hicho kimetoa maelekezo kwa jumuiya zake kuweza kujitegemea kiuchumi.
“Chama hichi kilitoa maelekezo kwa Jumuiya zake kuweza kujitegemea hivyo sisi kama UWT tumekuwa tukikimbizana ili kuhakikisha tunapata wawekezaji ili kuendeleza maeneo yetu nchi nzima,”amesema Mwegelo.
Amesema UWT wanampango wa kuzalisha mkaa mbadala unaotokana na mavumbi ya makaa ya mawe hivyo kutokana na wawekezaji huo kujikita zaidi kwenye teknolojia itawasaidia kutumia teknolijia hiyo katika uzalishaji.
Amesema katika miradi yote watahakikisha wanajielekeza katika kumuwezesha mwanamke hivyo chochote watakachoanzisha kitamgusa mwanamke moja kwa moja ili kuhakikisha wanamuinua kiuchumi.
“Tunajivunia kuwa na kundi kubwa la wanawake hivyo tunauwezo wa kuwafikia wanawake wote nchini hivyo tukijua hawa wawekezaji watakuja kuwekeza kwenye maeneo gani tutahakikisha tunawafikia wanawake husika kwani,”amesema.
Pia Mwegelo ametoa rai kwa wanawake nchini kuungana,kuwezeshana na kujengana kiuchumi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kufanya mambo makubwa katika uchumi wao na Taifa kwa jumla.
Ameongeza kuwa kwa sasa wapo kwenye usajili wa wanawake kote nchini kwenye mfumo wao hivyo hiyo itawasaidia kuendelea kuwaunganisha wanawake ili hata sera za nchi zilizowekwa ziweze kuwasaidia.
Kwa upande wake Mhandisi Anna Nyangasi wa Kampuni ya Canopus Energy Solutions amesema wawekezaji hao wamevutiwa na mpango wa UWT wa matumizi ya nishati mbadala hivyo watakapo kuja kwa ajili ya uwekezaji watajikita katika matumizi ya nishati mbadala kwa kutumia teknolojia ili kusapoti jitihada za Rais Dk.Samia.