Home KITAIFA DK. NCHIMBI ASISITIZA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA NI MAISHA YA WATU

DK. NCHIMBI ASISITIZA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA NI MAISHA YA WATU

Na Mwandishi wetu

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema uamuzi wa kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar ulizingatia kutanguliza mbele usalama wa maisha ya watu, maslahi, utulivu na mstakabali mwema wa Zanzibar, Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla, kuliko vyama vya siasa.

Hayo ameyasema leo Machi 24 Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akizungumza na Wazee wa Zanzibar, Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, ikiwa ni siku ya pili akiwa kwenye ziara ya kikazi, akitokea Pemba, ambako pia alifanya mazungumzo na mashauriano na Wazee wa Pemba, Machi 23, 2024.

Ameongeza kuwa uwepo wa Serikali hiyo Zanzibar umeondoa hali ya siasa za chuki na uhasama mkubwa uliokuwepo kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuundwa kwake, huku akisisitiza kuwa Chama hicho kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa uongozi kwa nchi ili kudumisha umoja na utulivu uliokusudiwa kwa maslahi ya Wazanzibar na Watanzania wote.

“Binafsi nikimsikia mtu anazungumzia kutaka kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, simwelewi huyo mtu hata kidogo. Kwa sababu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa kwa ajili ya usalama wa maisha ya watu, usalama wa Wazanzibar, usalama wa Watanzania maisha ya watu ni muhimu sana kuliko kitu chochote kwanza. Tuliweka mbele maslahi ya nchi, utulivu na umoja wetu, si vyama vya siasa.

“Mnakumbuka wakati fulani nikiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kila siku nenda rudi kwa helkopita kuja Zanzibar tulikuwa tunahangaika kuondosha uhasama na chuki Najua kuna wakati wenzetu wanapata gadhabu na kuzungumza kwa jaziba sisi wana CCM tusiende huko hata kidogo Sisi ndiyo chama tawala sisi ni walezi mlezi hasusi tusiache wajibu wetu wa kulea hata kidogo mtoto ndiye anasusa na katika hili naombeni sana wazee wote wa Zanzibar na Tanzania, mniunge mkono,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.

Pia amesisitiza msimamo wa CCM kuendeleza kutimiza wajibu wa kipekee wa kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na misingi yake, ndio Iliyowaweka watu wote kuwa sawa mbele ya sheria na kuondoa kila aina ya ubaguzi, ukiwemo wa matabaka, rangi na hali ya mtu.

“Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yameondoa matabaka yakaleta utu, sote tunaunganishwa na utu wetu tunao wajibu wa kipekee kuhakikisha tunaendelea kulinda misingi ya mapinduzi tuko tayari kuendelea kulinda hakuna umbo au rangi au hali inampatia haki zaidi mtu mwingine kuliko mwingine ukifanya ubaguzi wa namna hiyo wewe ni kaburu tun a ukaburu hauna rangi huo ndiyo msimamo wa CCM,” amesema.

Akiwakaribisha katika mazungumzo hayo, Dk. Nchimbi aliwaambia Wazee wa Zanzibar kuwa wao ni mashahidi jinsi ambavyo awamu tofauti tofauti za Serikali za CCM, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimefanya kazi kubwa ya maendeleo ya watu na vitu, akiwakumbusha kuwa wasisite kuendelea kutoa ushauri au maelekezo ili kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza kwa kuzingatia misingi ya kuundwa na kuanzishwa kwake, ikiwemo kuwatumia watu na kubadili hali yao ya maisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here