Home KITAIFA MATINYI AMESEMA UCHUMI WA TANZANIA UMEENDELEA KUKUA LICHA YA ATHARI KUBWA...

MATINYI AMESEMA UCHUMI WA TANZANIA UMEENDELEA KUKUA LICHA YA ATHARI KUBWA ZA UVIKO-19

Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Idara ya Habari
Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mlipuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na Mashariki ya Kati.

Hayo ameyasema leo Machi 24 jijini Dar es Salaam na Matinyi wakati akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari akitoa mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema matatizo hayo yaliutikisa uchumi wa Tanzania uliokuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 7 na kuushusha hadi asilimia 4.2 mwaka 2020.

Amesema hivi sasa ukuaji wa uchumi umefikia asilimia 5.2 kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka
(GNI per capita) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080,
lakini mwaka 2022 ni dola 1,200,”amesema.

Amesema Serikali imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya asilimia 4 kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC).

Vile vile, amesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba mwaka 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4, akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4.

Ukusanyaji Mapato

Matinyi akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato amesema Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri ambapo katika kipindi cha
miaka mitatu makusanyo yamefikia shilingi trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23
kutoka shilingi trilioni 18.15 mwaka 2020/21 sawa na ongezeko la trilioni
5.99.

“Kwa Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni shilingi trilioni 2.13.

“Hadi kufikia Machi 20, 2024 TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha shilingi trilioni 19.21, ikiwa ni dalili kwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita,”amesema.

Kuhusu uwekezaji Matinyi amesema katika kipindi cha Machi 2021 hadi Machi 2024, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464.

Amesema kati ya miradi hiyo asilimia 35 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 41 ni ya Wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya Watanzania na Wageni.

Ofisi ya Msajili wa Hazina

Akizungumza kuhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina Matinyi amesema thamani ya
uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina
imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76
mwaka 2023 sawa na ongezeko laa asilimia 8.6.

Amesema sababu la ongezeko hilo ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.

“Ofisi pia imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023,
sawa na ongezeko la asilimia 58.

“Serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi asilimia 37 huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia16 zisizohamishika katika kampuni za madini,”amesema.

Sekta ya Madini

Kuhusu sekta ya Madini Matinyi amesema kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2024, Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza
sekta hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada
mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha shilingi trilioni 1.93.

Amefafanua kuwa awali mwaka 2021/22 ilikuwa Shilingi bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia sh bilioni 690.4.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa shilingi bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia shilingi
bilioni 476.8.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here