Na Mwandishi wetu
MIEZI minne baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia hospitali kubwa zaidi ya Gaza, al-Shifa, wakidai kuwa ni kificho cha kamandi ya Hamas na kituo cha udhibiti, wamerejea.
Jeshi la Israel limesema lilikuwa na “intelijensia halisi” kwamba watendaji wa Hamas wamejipanga tena huko. Wapalestina wameiambia BBC kuhusu hofu yao ya kunaswa katika vita vikali.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kwamba inaonesha haja kubwa ya mkakati wa kina wa kukabiliana na kundi la wapiganaji wa Kiislamu na mpango wazi juu ya utawala wa baada ya vita wa Gaza.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) sasa linadai kuwa limewaua “zaidi ya magaidi 140” katika mapigano yanayoendelea huko al-Shifa na kuwatia mbaroni watu 600, wakiwemo makumi ya makamanda wakuu wa Hamas na wengine kutoka Islamic Jihad. Wanajeshi wawili wa Israel pia wameuawa.
Ripoti za Israeli zinaonesha kuwa katika wiki za hivi karibuni jeshi liligundua kuwa Hamas walianza tena operesheni huko al-Shifa na kwamba wengine walipeleka familia zao hospitalini. IDF inasema iligundua akiba ya silaha na kiasi kikubwa cha fedha kwenye eneo hilo.
Hamas imekanusha kuwa wapiganaji wake walikuwa wamejikita huko na kudai kuwa waliouawa walikuwa wagonjwa waliojeruhiwa na watu waliokimbia makazi yao.
Mashahidi wa Kipalestina wameiambia BBC kwamba milio ya risasi na mashambulizi ya anga ya Israel yamekuwa yakihatarisha wagonjwa, matabibu na mamia ya watu ambao bado wanajihifadhi katika eneo hilo.
Mwandishi wa habari wa eneo hilo wamechapisha video ya moshi unaofuka kutoka kwenye jumba hilo.
Katika video nyingine ambayo haijathibitishwa, iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, makumi ya wanawake wanaonekana wakiwa wamelala kwenye jengo pamoja na watoto wao. Mmoja anasema: “Waliwapeleka wanaume wetu mahali pasipojulikana na sasa wanawataka wanawake na watoto kuondoka. Hatujui tutakwenda wapi”.
Afisa wa IDF amesema kwa vipaza sauti: “Usiondoke kwenye majengo bila maelekezo. Tunatafuta kuwahamisha raia bila madhara, kama tulivyofanya katika hospitali nyingine hapo awali.”
Tangu Jumatano jioni, mawasiliano yamewekewa vikwazo vikali, na hivyo kufanya kuwa vigumu kuwasiliana na madaktari na wengine katika eneo la tukio.
Chanzo BBC.