Na Scolastica Msewa, Kibaha
WANANCHIi zaidi ya 6000 wamejitokeza kupata huduma ya afya ya kinywa na meno mkoani Pwani Katika kipindi cha wiki Moja ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya afya ya kinywa na meno ambapo Wataalamu wa afya ya kinywa na meno zaidi ya 80 wamekuwa wakitoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kibaha Rais wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA) Dk. Gema Belege amesema Wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwaajili ya maadhimisho hayo duniani ambayo huadhimiswa Kila mwaka Machi,20 ambapo kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika mjini Kibaha mkoani Pwani.
Amesema Wataalamu hao 80 wamekuwa rasmi mkoani humo kutoa huduma ya afya ya kinywa na meno kwa Wananchi wa mkoa huo ambapo wamekuwa na kambi tatu katika vituo vya huduma katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi, hospitali ya Wilaya ya Lulanzi na katika Kituo cha afya cha mkoani.
“Lakini pia tunetembelea shule za msingi tisa, vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu saba ambako tumetoa elimu na kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno na waliobainika kuhitaji matibabu tumewapeleka kwenye kambi za afya hizi tatu kwaajili ya kupatiwa huduma za afya.
“Mwitikio umekuwa ni mkubwa sana kwani mpaka sasa tumeshahudumia Wananchi zaidi ya 6000 katika sehemu zote hizo za mashule, vituo vya kutolea huduma na kwenye vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu,”amesema Dk. Gema .
Amesema tatizo kubwa ambalo wameliona kwa wateja wengi walipofikia ni ugonjwa wa kuoza meno, matatizo mengine ni pamoja na magonjwa ya fizi, mpangilio mbaya wa meno na ukosefu wa meno au wanaita mapengo.
“Huduma ambazo tumekuwa tukizitoa ni pamoja na elimu ya afya ya kinywa na meno, matibabu ya kuziba meno, kuziba meno kwa meno yaliyohusisha kuziba Hadi kwenye milija ya fahamu, kusafishwa meno maalufu kama kuondoa ugaga uchafu ulioganda kwenye meno na huduma ya meno bandia ya aina ya kuvaa na kuvua,”ameongeza.
DK. Gema amesema hadi leo wameweza kutoa meno bandia bure kwa wagonjwa zaidi ya 133 yaani Wananchi wote waliopata huduma kwenye maadhimisho hayo wamepata huduma bila malipo yoyote.
“Tunaishukuru sana serikali na wizara za afya na TAMISEMI kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta kutuletea miundombinu mipya, mizuri na yakisasa na Wataalamu wanatoa huduma za kisasa na wametusaidia kufikisha Wataalamu wa afya hapa ili watoe huduma kwa wananchi,” amesema.
Amefafanua kuwa iwapo utatunza afya ya kinywa na meno vizuri pia utatunza afya ya mwili mzima maana Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya meno na afya ya mwili mzima kwa ujumla kwahiyo wanawasihi wananchi wazidi kutembelea vituo vvya afya ili watumie fursa hiyo ambayo serikali imewekeza
“Kama mtu ameona tatizo lolote la afya ya kinywa na meno asiende kwenye duka la dawa akaanza kutumia madawa kwa kupokea maelekezo yasiyoyakitaalamu bali waende kwa Wataalamu ili wakawachunguze, kuwashauri na kuwapa tiba sahihi kwasababu vifaa vipo na Wataalamu pia wapo,”amesema.