Home BIASHARA DKT. NCHEMBA ATETA NA UONGOZI WA BENKI YA WATU WA ZANZIBAR

DKT. NCHEMBA ATETA NA UONGOZI WA BENKI YA WATU WA ZANZIBAR

Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu  Nchemba, ameipongeza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kupanua biashara zake hapa nchini na kuitaka Benki hiyo ishushe zaidi riba ili wananchi wakiwemo watumishi wa Umma waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki hiyo.


Hayo ameyasema leo Machi 20  jijini Dodoma Dk. Nchemba  alipokutana na Uongozi wa Benki hiyo Ofisini kwake  ambapo walijadili namna Benki na Serikali zinaweza kushirikiana kukuza uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi.


“Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za Benki hii kwa kuhakikisha kuwa wananufaika na mazingira ya ufanyaji biashara katika Sekta hiyo ya fedha,”amesema Dk. Nchemba.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Benki hiyo,  Said Mohamed Said, amesema kuwa Benki yake imeendelea kukua na kupanua huduma zake upande wa Tanzania Bara, katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Dodoma na kwamba hivi karibuni inatarajia kufungua matawi mengine katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tanga na Arusha.


Amesema kuwa Benki yake imeendelea kukua na katika kipindi cha miaka mitatu sasa ilipata faida ya shilingi bilioni 75 kabla ya kulipa kodi, ina mali zisizohamishika zenye thamani ya shilingi trilioni 2 na katika kipindi hicho imetoa mikopo inayofikia zaidi ya shilingi bilioni 194.


Ameiomba Wizara ya Fedha iisaidie Benki hiyo iingizwe kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki wa GePG, kwa ajili ya kukusanya malipo ya Serikali na kuangalia namna ya kupunguza baadhi ya gharama ili waendelee kutoa mikopo kwa riba nafuu kwa wateja wao kama ilivyodhamira ya Benki hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here