Home KITAIFA TANZANIA NA BURUNDI ZAJADILIANA UJENZI WA SGR.

TANZANIA NA BURUNDI ZAJADILIANA UJENZI WA SGR.

Na Joseph Mahumi na Josephine Majura, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Miundombinu wa Burundi Dieudonné Dukundane, kuhusu maendeleo ya Mradi wa Reli ya Kisasa SGR utakaoziunganisha nchi hizo mbili.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Dodoma, Viongozi hao wamesema kuwa mradi huo utakapokamilika utachochea biashara ya madini na kilimo pamoja na kuimarisha mahusiano ya kikanda na kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.


Dk. Nchemba amesema kuwa Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika maandalizi ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) umekua mzuri na kwamba watalaamu wa pande zote mbili wameendelea na vikao hususan katika eneo la manunuzi na fedha ili kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa.


“Ujenzi wa Reli hii ya Kisasa ya kuunganisha nchi zetu ni muhimu sana kwetu na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni mradi wa Kipaumbele na anataka ukamilike,” ameongeza Dk. Nchemba.


Amesema kuwa wataalum kutoka nchi hizo mbili wanaendelea kushirikiana ili kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa na kufikia matarajio ya Rais wa Tanzania pamoja na Rais wa Burundi ya kuona mradi huo unafanikiwa.


Naye Waziri wa Miundombinu na Makazi wa Jamhuri ya Burundi, Dieudonné Dukundane, alisema kuwa nchi yake itahakikisha kuwa mradi huo unapewa kipaumbele na tayari timu ya wataalam kutoka Burundi ipo Dar es Salaam ikiendelea kupitia masuala ya manunuzi wakishirikiana na wataalam wa Tanzania.


“Rais wangu Evariste Ndayishimiye, ametuelekeza kuwa tufuatilie kwa ukaribu na kwa kipaumbele mchakato mzima unakwenda kama ilivyopangwa ili uishe vizuri, na mimi nimeishi hapa Tanzania kwa miaka sita nimeona namna ambavyo SGR itakavyoharakisha maendeleo ya nchi,” amesema Dukundane.

Mradi huo wa Reli ya Kisasa (SGR) baada ya kukamilika hususan Ujenzi wa Reli ya Uvinza hadi Musongati nchini Burundi kutawezesha kusafirisha tani milioni 3 za madini kwa mwaka kutoka mgodi mkubwa wa madini ya Nickel uliopo Musongati nchini Burundi unaokadiriwa kuwa na hifadhi ya tani milioni 150 za madini ya Nickel, Cobalt na Copper, na pia kuimarisha shughuli za kiuchumi za nchi hizo mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here