Home KIMATAIFA ZUMA AJIPANGA KUKIONDOA CHAMA CHA ANC MADARAKANI.

ZUMA AJIPANGA KUKIONDOA CHAMA CHA ANC MADARAKANI.

LICHA ya kuwa Rais wa zamani aliyehangaishwa na kupelekwa jela, Jacob Zuma anageuka kuwa mwanasiasa asiyetabirika katika kampeni za uchaguzi nchini Afrika Kusini.

Hii inafuatia uamuzi wake wa kukihama Chama Tawala cha African National Congress (ANC) na kujiunga na Chama Kipya cha Umkhonto we Sizwe, kumaanisha Spear of the Nation.

Zuma mwenye umri wa miaka 81 anaongoza kampeni zake katika Uchaguzi Mkuu wa Mei 29, akiwataka watu kukipa kisogo chama cha ANC kinachoongozwa na mrithi wake, Rais Cyril Ramaphosa.

“Zuma hataki mamlaka, lakini kujiinua katika ANC. Anataka kumng’oa Ramaphosa ili apate kiongozi anayekubalika zaidi,” mchambuzi wa kisiasa Richard Calland aliambia BBC..

Kura mbili za maoni za hivi punde zaidi zinaonyesha kuwa chama cha Zuma – kinachojulikana kwa kifupi cha MK – kinapata ushawishi mkubwa, kwa kupata karibu asilimia 13 ya kura za kitaifa na asilimia 25 katika ngome ya kisiasa ya rais huyo wa zamani ya KwaZulu-Natal.

Chama cha MK kinatarajia kushikilia mizani ya madaraka, hasa huku kura za maoni mbalimbali zikionyesha kuwa ANC inaweza kupoteza wingi wake wa moja kwa moja katika bunge la taifa kwa mara ya kwanza tangu kilipochukua mamlaka mwishoni mwa utawala wa wazungu wachache miongo mitatu iliyopita.

Hapo awali, ANC ilipuuza kuundwa kwa chama cha MK lakini baada ya Bw Zuma kuweka uzito wake nyuma yake mwezi Desemba, chama hicho kilianzisha hatua za kisheria katika mahakama ya uchaguzi kukifutia usajili na kukizuia kushiriki.

Pia inataka Mahakama Kuu kukizuia kutumia jina la MK, ikisema kuwa ANC ina hakimiliki yake.

Vita juu ya jina hilo ni muhimu, kwani MK inarejelea mrengo wa ANC ambao Nelson Mandela alianzisha mnamo 1961 kupigana na mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Kwa hivyo, ina ishara kubwa ya kisiasa, na ANC imedhamiria kumzuia Bw Zuma – ambaye alijiunga na mapambano ya kijeshi ya ANC akiwa kijana.

Chama cha MK kimemweka Bw Zuma katika orodha ya kwanza ya wagombea ubunge, licha ya kwamba Tume Huru ya Uchaguzi ilisema mwezi Januari kwamba kuhukumiwa kwake kulimuondoa.

Binti ya Bw Zuma, Duduzile Zuma-Sambudla, pia ameteuliwa kuwa mgombea ubunge na chama cha MK, na kupendekeza kuwa rais huyo wa zamani anamwona kama mrithi wake wa kisiasa na mlezi wa urithi wake.

Chanzo;BBC.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here