Na Mwandishi wetu
BARAZA la Ushauri la Watumiaji Huduma za Anga (TCAA CCC) limeahidi kuanza kutumia Teknolojia ya akili mnemba “Artificial intelligence ” ili kusogeza karibu huduma za usafiri wa anga.
Akizungumza Machi 13 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Haki za Mtumiaji Duniani Katibu Mtendaji TCAA -CCC, Innocent Kyara amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha utoaji huduma kwa umma kupitia matumizi ya teknolojia.
“TCAA CCC ikiwa ni miongoni mwa taasisi za umma yenye wajibu wa kutekeleza mpango huu wa serikali tumejimpanga kuanza kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI) kutoa elimu na kusambaza taarifa mbalimbali kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga na umma kwa ujumla,”amesema Kyara.
Amesema teknolojia hiyo ina tija kwa sababu mtumiaji wa huduma za usafiri wa anga watapata taarifa muhimu za safari kupitia”chatbot” na kupata mrejesho kwa haraka na urahisi.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kwa namna ya mdahalo ambapo wadau mbalimbali kutoka sekta ya usafiri anga, ardhini, mawasiliano, maji na nishati watajadiliana namna ya teknolojia akili mnemba inavyoweza kuawaathiri watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na zisizothibitiwa hapa nchini.
” Teknolojia hii ni mpya ugunduzi na maendeleo ya teknolojia hii hufanyika kwa kasi nasi hatuna budi kwenda na kasi hiyo ili kuhakikisha tunakua na kesho yenye haki na salama kwa watumiaji nchi,”ameongeza.
Aidha amewakaribisha wadau mbalimbali na umma kwa ujumla ili waweze kujadiliana mazuri ya akili mnemba pamoja na namna gani wanaweza kukabiliana na athari hasi zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya akili mnemba.
Maadhimisho ya Siku ya Haki Watumiaji Duniani yatanyika machi 15 mwaka huu mgeni rasmi anatarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na kauli mbiu “Akili Mnemba” Artificial Intelligence Inayozingatia haki na uwajibikaji wa mtumiaji.