Home KITAIFA PURA Na DMI KUSHIRIKIANA

PURA Na DMI KUSHIRIKIANA

Na Esther Mnyika

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa kushirikiana na Chuo cha Bahari Dar es salaam(DMI) katika kuhakikisha inamsaidia mwananchi kupata ajira katika shughuli za bahari wamekubaliana kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kushiriki katika utafiti wa bahari kuu lakini pia kutoa huduma kwenye bahari.

Akizungumza leo March 13,2024 jijini Dar es salaam  wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ushirikiano kati ya PURA na DMI Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni amesema kumekuwa na fursa nyingi za ajira kwa watanzania hivyo ili kuweza kufanyakazi kwenye kina kirefu cha bahari ni lazima kupata mafunzo yanayohusu usalama.

“Katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kwenye kinakirefu cha bahari kunakuwa na shughuli mbalimbali lakini pia huduma nbalimbali zinahitajika kama chakula sasa mtu huwezi kufanya kazi  hata ya usafi na kupeleka chakula kama utakuwa ujapata mafunzo kwa hiyo tumeshirikiana ili kuhakikisha watanzania wanapata mafunzo na kuchangamkia fursa zinazojitokeza baharini,” amesema Mhandisi Sangweni.

Amesema awali walikuwa wanapeleka wataalam kusoma nje ya nchi na ilikua gharama kubwa inatumika kwani mtu mmoja alikua anatumia mpaka dola 7000 sawa na milion 15 kwa mafunzo ya wiki moja hivyo kwa kuanzisha mafunzo hayo kutapunguza gharama.

Amesema watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwani kuna miradi mingi inatarajiwa kuanzishwa ukiwemo wa mradi wa LNG.

Aidha wameiomba serikalini kuweza kuwaunga mkono ili waweze kutekeleza mradi huo kama walivyokusudia kuhakikisha elimu na mafunzo ya maswala ya bahari inatolewa kwa haraka na ufanisi.

Naye Mkuu wa Chuo cha DMI, Tumaini Gurumo amesema makubaliano hayo yatasaidia watanzania kupata elimu na kuweza kuajilika katika nafasi mbalimbali katika shughuli za baharini.

Amesema chuo kinawataalam hivyo wataongeza wataalam zaidi ili kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwa weredi hapa hapa nchini kwani kozi nyingi za bahari huwa zinatolewa.

“Tunakwenda kutoa mafunzo kwa watanzania mafunzo haya yatawasaidia kwenye usalama wao pindi zinapotokea fursa kwenye bahari za kwenda kutoa huduma mbalimbali,”Amesema Gurumo.

Gurumo ametoa rai kwa Watanzania kuanza kufikiri namna ya kumiliki meli za kubeba mafuta yanayotafutwa hapa nchini ili kuhakikisha wanatumia kwa faida bahari.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PURA,  Halfani Halfani amesema taasisi zetu zinatekeleza kwa vitendo azima ya serikali ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika shughuli za utafutaji,uchimbaji na uendelezaji wa miradi ya gesi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya DMI,  Kapteni Ernest Bupamba amesema shughuli za uchimbaji na utaftaji wa mafuta na gesi zinahitaji umakini mkubwa kwani uzembe wowote ukijitokeza unaweza kughalimu mradi mzima na ukizingatia kuwa miradi hiyo hutumia gharama kubwa.

Mwishoo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here